STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 31, 2012

Kocha wa Simba sasa kutua leo Yanga wafika salama Uturuki


UONGOZI wa Simba umedai kuwa kocha mpya wa timu yao, Mfaransa Patrick Lieweg atawasili kwenye Uwanja wa Kiamataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) leo saa 7:15 mchana akitokea mjini Baho, Ufaransa.
Ujio wa kocha huyo umekuwa wa danadana tangu ilipotangazwa awali angetua Desemba 27, lakini safari hii uongozi umethibitisha kuwa atatua leo mchana bila kupepesa macho.
Akizungumza na MICHARAZO jana, Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alisema kuwa kocha huyo atatua kurithi mikoba ya aliyekuwa kocha wao, Mserbia Milovan Cirkovic, ambaye wamelazimika kumfungashia virago baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
“Kulikuwa na tatizo la usafiri wa ndege katika nchinnyingi za Ulaya kipindi hiki cha bararidi kali barani humo ndiyo maana alikuwa anakosa ndege za kumleta Tanzania,” alisema Rage.
Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi hiyo, walilazimika kuvunja mkataba na Cirkovic kutokana na kilichodaiwa na uongozi wa klabu hiyo kuwa kocha huyo alikuwa ‘anaikamua’ kiasi kikubwa mno cha fedha.
Hata hivyo, baada ya kuvunja mkataba na kocha huyo aliyewapa ubingwa msimu uliopita, ‘Wekundu wa Msimbazi’ tayari wameingia mkataba na makocha wawili wapya, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Mganda Mosses Basena.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, baada ya kutua kwa Lieweg, uongozi wa klabu hiyo utatangaza mfumo mpya wa benchi la ufundi la timu yao.
Katika hatua nyingine msafara wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga umefika salama nchini Uturuki na unatarajiwa kuanza programu zao nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa klabu hiyo, kikosi hicho kilifika salama jana asubuhi na leo kilitarajiwa kuanza kujifua kabla ya kuanza kucheza mechi kadhaa za kirafiki na wenyeji wao zikiwa maalum kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara na utetezi wao wa Kombe la Kagame litakalofanyika nchini Rwanda.

No comments:

Post a Comment