STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 31, 2012

Minziro atamba Yanga moto ule ule

Fred Minziro (kulia) katika moja ya majukumu yake uwanjani

KOCHA Msaidizi wa klabu ya Yanga, Fred Felix Minziro, ametamba kwamba moto waliomalizia nao kwenye duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara, ndiyo watakaoanza nao katika duru lijalo, huku akisisitiza lazima Yanga iwe bingwa 2012-2013.
Aidha kocha huyo ametamba kwamba timu yao imejipanga ili kuhakikisha wanatetea taji lao la Kombe la Kagame katika michuano itakayofanyika hivi karibuni nchini Rwanda.
Akizungumza na MICHARAZO kabla ya kupaa na timu kwenda Uturuki, Minziro, beki wa kimataifa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alisema ubora wa kikosi alichonacho na namna  wanavyojiandaa, inampa imani ya kuamini kwamba Yanga itawavua ubingwa wa ligi watani zao, Simba msimu huu.
Minziro, alisema Yanga itaendeleza moto ule ule waliomalizia nao duru la kwanza la ligi hiyo iliyowatoa nafasi za kati mpaka kileleni ikiwaengua waliokuwa vinara Simba na Azam, ili mwisho wa msimu klabu yao iwe mabingwa wapya wa Tanzania.
"Hatudhani kama tutaanza kinyonge kama ilivyokuwa katika duru la kwanza, tupo katika maandalizi kabambe ili kuhakikisha tunaendeleza moto na kasi yetu ili kurejesha taji tuliloporwa na watanbi zetu, Simba," alisema Minziro.
Minziro, alisema japo anatambua duru lijalo litakuwa lenye ushindani mkubwa, lakini wao wamejiandaa vya kutosha kuhakikisha wanafanya vema, huku akisisitiza kuwa maandalizi yao yanalenga pia kwenda kutetea taji lao la Kombe la Kagame njini KIgali.
"Macho na akili zetu zote tumezielekeza kwenye duru la pili la ligi pamoja na michuano ya Kagame, tungependa kwenda kutetea taji ugenini, tunajiamini na wachezaji wana ari kubwa ya kufanya hivyo," alisema Minziro.
Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 29, tano zaidi ya Azam waliopo nafasi ya pili na sita zaidi ya watani zao Simba wanaoshika nafasi ya tatu, ilitwaa taji hilo la Kagame Julai, 2012 kwa kuilaza Azam mabao 2-0 katika mchezo fainali zilizochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment