STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 9, 2013

Sikinde yapeleka Jinamizi lake Sauti za Busara

Waimbaji wa Mlimani Park, Hassan Kunyata, Abdallah Hemba na Hassan Bichuka wakiwajibika

BENDI kongwe ya muziki wa dansi, Mlimani Park 'Sikinde' inatarajiwa kuondoka jijini Dar keshokutwa kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kushiriki tamasha la kimataifa la muziki la Sauti za Busara litakalofanyika visiwani humo kuanzia Alhamisi.
Katibu wa Sikinde, Hamis Milambo aliiambia MICHARAZO kuwa, bendi yao ni miongoni mwa makundi ya muziki na wasanii walioalikwa kushiriki tamasha hilo linalofanyika kila mwaka visiwani Zanzibar.
Alisema bendi yao imejiandaa kwenda kutoa burudani kabambe sambamba na kujitangaza kupoitia tamasha hilo ambalo hushirikisha wasanii na makundi ya muziki kutoka nchi mbalimbali za Kiafrika.
"Bendi yetu imeteuliwa kushiriki tamasha la kimataifa la muziki la Sauti za Busara na tunatarajiwa kuondoka Jumanne kuelekea Zanzibar tukiwa tumekamilika na kutaka kuwaonyesha makundi mengine kwamba sisi ndiyo Mabingwa wa dansi," alisema.
Sikinde itaungana na wasanii wengine wa Tanzania katika tamasha hilo litakalofanyikia eneo la Ngome Kongwe, akiwamo Peter Msechu, Msafiri Zawose & Sauti Band, Super Maya Baikoko, Lumumba Theatre Group na Culture Musical Club.
Makundi mengine yatakayoshiriki tamasha hilo litakalomalizika Februari 17 ni Cheikh Lo (Senegal), Khaira Arby (Mali), Comrade Fatso na Chabvondoka (Zimbabwe), Atongo Zimba (Ghana), N'Faly Kouyaté (Guinea), Nathalie Natiembe (Reunion), Nawal & Les Femmes de la Lune na (Comoros/Mayotte).
Pia wamo Wazimbo (Msumbiji), The Moreira Project (Msumbiji/Afrika Kusini), Owiny Sigoma Band (Kenya/UK), Mokoomba (Zimbabwe), Mani Martin (Rwanda), Burkina Electric (Burkina Faso/USA) na Sousou & Maher Cissoko (Senegal/Sweden).
Kwa mujibu wa waandaaji wa tamasha hilo pia litajumuisha filamu za muziki wa Kiafrika, kumbukumbu, video za muziki na maonesho ya moja kwa moja, yote yakilenga kukuza utajiri na utofauti wa muziki wa Kiafrika.

No comments:

Post a Comment