STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 14, 2013

Arsenal yang'oka Ulaya, Malaga yaisulubu Porto

Mfungaji wa bao la pili la Arsenal, Laurent Koscielny (kulia) akiwa haamini kama wametoka michuano ya UIaya
 LICHA ya kupata ushindi uliotarajiwa wa mabao 2-0 ugenini nchini Ujerumani, Arsenal ya Uingereza imejikuta ikishindwa kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa jana.
Arsenal ilikuwa nchini humo kukabiliana na wenyeji wao Bayern Munich ikiwa nyuma ya mabao 3-1 iliyonyukwa katika pambano lao la awali lililochezwa mjini Londoni mwishoni mwa mwezi uliopita.
Ushindi huo uliotokana na mabao ya Olivier Giroud aliyefunga dakika ya tatu tu ya kuanza kwa mchezo huo na lile la kipindi cha pili lililotumbukizwa wavuni na Laurent Kocsielny, ulifanya matokeo ya mwisho kuwa sare ya mabao 3-3, lakini vijana hao wa Arsene Wenger kung'oka kwa faida ya bao ya ugenini.
Tofauti na mechi yao ya London, Arsenal jana walionyesha uhai na kuwafunika wenyeji wao na kuwashutukiza kwa bao hilo la mapema la Giroud lililodumu hadi wakati wa mapumziko.
Arsenal ilisubiri hadi dakika nne kabla ya kumalizika kwa pambano hilo kuongeza bao la pili kupitia kwa Laurent Koscielny aliyefunga kwa kichwa ambalo hata hivyo halikusaidia kusonga mbele ili kukaribia ndoto zao za kumaliza ukame wa mataji klabuni hapo.
Michuano hiyo ndiyo iliyokuwa tumaini pekee la Arsenal kumaliza ukame huo wa mataji kwani ilishatolewa kwenye michuano ya Kombe la Ligi, Kombe la FA na ndoto za kutwaa ubingwa wa Ligi ya England ni finyu kutokana na ukweli imeachwa mbali kipointi na vinara wa ligi hiyo, Manchester United.
Katiika mechi nyingine ya usiku wa jana katika michuano hiyo ya Ulaya, Malaga ya Hispania ikiwa nyumbani ililipa kisasi cha kunyukwa na Porto ya Ureno bao 1-0 kwa kuilaza wageni wao hao mabao 2-0 na kutinga robo fainali.
Malaga ilipata mabao yake kila kipindi kupitia kwa nyota wake, Isco aliyefunga la kwanza dakika ya 43 na Roque Santa Cruz kuonyesha la pili katika dakika ya 77 na kuifanya timu hiyo sasa kuungana na timu za Barcelona na Real Madrid kutoka Hispania, Borussia Dotmund na Bayern Munich za Ujerumani, PSG ya Ufaransa na Galatasaray ya Uturuki kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment