STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 14, 2013

Mashabiki Man U, Real wachapana risasi Dar

Timu za Real Madrid na Manchester zilizoumana hivi karibuni na kupelekea mashabiki wa soka nchini kutwangana  risasi


NI kama hadithi lakini huu ndiyo ukweli; soka limekuwa likiibua hisia kali miongoni mwa wanaolifuatilia kiasi cha baadhi ya mashabiki kufikia hatua ya kujiua ama kusababisha maafa kwa wengine!
Ubishani wa soka baina ya mashabiki wa klabu za Manchester United ya England na Real Madrid ya Hispania umezua balaa la aina yake katika eneo la Sinza Kumekucha jijini Dar es Salaam baada ya mmoja wa mashabiki hao kumtwanga risasi mwenzake wakati wakifuatilia kupitia luninga mechi ya marudiano ya hatua ya 16-bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ambapo Real iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saam jana, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kuwa shabiki wa soka aliyepigwa risasi na kujeruhiwa mkononi ni David Kweka (32) na anayedaiwa kumpiga risasi ni shabiki mwingine wa soka aitwaye Robert Wambura.
Kamanda Kenyela alisema kuwa tukio hilo lilitokea Jumanne iliyopita wakati wawili hao walipokuwa wakifuatilia mechi kati ya Manchester United na Real Madrid iliyoanza saa 4:45 usiku (kwa saa za Tanzania).
Aliongeza kuwa majeruhi (Kweka) aliumia baada ya kupigwa risasi katika kiganja chake cha mkono wa kulia na Wambura ambaye anamiliki silaha hiyo kihalali, chanzo kikitajwa kuwa ni mabishano makali kati yao kuhusiana na mechi hiyo.
Alisema kuwa jeshi hilo linamshikilia Wambura na silaha iliyotumika na kwamba muda wowote (kuanzia jana) atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomakabili.
“Ni jukumu la Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba tunaweka ulinzi katika maeneo ya mikusanyiko ya watu wengi, hivyo tumejipanga kukabiliana na matukio kama hayo yanayotokea katika maeneo mbalimbali, hasa katika maeneo wanayoonyesha mpira ili kuondokana na ushabiki unaoleta madhara,” alisema Kenyela.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Old Traford, England, wenyeji Manchester United walichapwa 2-1 na magoli ya Real inayoongozwa na kocha Jose Mourinho yalifungwa na Luka Modric na Cristiano Ronaldo huku goli pekee la Man U likitokana na kujifunga kwa beki Sergio Ramos wa Real.
Matokeo hayo yaliipa nafasi Real kutinga robo fainali kwa jumla ya magoli 3-2 kwani katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu nchini Hispania, timu hizo zilitoka sare ya 1-1.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment