STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 20, 2013

Kocha Polisi Tabora achekelea kuiokoa timu


KOCHA wa timu ya soka ya Polisi Tabora, Mwinyimadi Tambaza amesema amefurahishwa kufanikiwa kuiokoa timu yake iliyokuwa katika hali mbaya na kusalia kwenye Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Polisi Tabora iliyomaliza duru la kwanza la ligi hiyo ikiwa na pointi tatu tu imenusurika kushuka daraja baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba ya Mwanza katika mechi yao ya kufungia msimu wa ligi hiyo.
Ushindi huo uliifanya timu hiyo kuweza kuokoka kuteremka daraja na kuiacha Morani ikiungana na timu nyingine mbili ikiwamo Moro United na Small Kids kushuka hadi Ligi Daraja la Pili.
Akizungumza na MICHARAZO juzi, Tambaza alisema anashukuru vijana wake kutekeleza kila alichokuwa akiwafundisha na kujituma uwanjani kiasi cha kuiwezesha kuiokoa Polisi kutoshuka daraja kwa hali mbaya iliyokuwa nayo.
Kocha huyo alisema mafanikio aliyoyapata kwa kuweza kuisaidia Polisi kuvuna pointi 15 katika duru la pili ni furaha kwake kwa vile ameweza kutimiza ahadi yake ya kuiokoa timu hiyo isishuke daraja.
"Wakati nikiitwa kuja kuinoa Polisi ilikuwa katika hali mbaya, ila nilijipa moyo nikijiamini kwa uwezo niliokuwa nao kwa kuahidi nitapigana kufa na kupona kuiokoa iishuke daraja na imekuwa kweli ni faraja kwangu," alisema.
Alisema baada ya kuinusuru timu hiyo anafanya utaratibu wa kuwasilisha ripoti na mapendekezo yake kwa mabosi wake ili waanze kujipanga mapema kwa ajili ya msimu ujao akiwa na ndoto na kuipandisha Ligi Kuu Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment