STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 7, 2013

TFF yabanwa na serikali, hofu yatanda


Waziri Dk Mukangara

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ameliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha kuwa linaitisha uchaguzi wake mkuu kabla ya Mei 25 mwaka huu; amri ambayo inazidi kuiweka Tanzania katika hatari ya kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambalo haliruhusu masuala ya soka kuingiliwa na serikali.
Amri hiyo ni moja kati ya maagizo matatu yaliyotolewa na serikali katika kikao cha pamoja kilichofanyika jana baina ya viongozi wa wizara, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na TFF.
Kikao hicho kilichofanyika jana asubuhi badala ya leo kama TFF walivyokuwa wameomba katika barua yao ya Jumatatu Februari 4 kilihudhuriwa na Dk. Mukangara, naibu wake Amos Makalla, katibu mkuu wa wizara Seth Kamuhanda, mkurugenzi wa michezo Leonard Thadeo, mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi na katibu wa BMT, Henry Lihaya.
TFF iliwakilishwa na katibu mkuu Angetile Osiah, mjumbe wa kamati ya utendaji Alex Mgongolwa na mkurugenzi wa ufundi, Sunday Kayuni.
Baada ya kikao hicho, Dk. Mukangara aliwaambia waandishi wa habari kuwa amewaandikia barua TFF kuwapa maagizo matatu aliyoyataja kuwa ni; kuhakikisha shirikisho hilo la soka linatangaza hadharani kuwa limekubaliana na maelekezo yaliyotolewa na wizara na kwamba tamko hilo litolewe kabla ya Machi 11 mwaka huu.
Barua hiyo ambayo ilionwa nakala yake jana imeitaka TFF katika agizo la pili kuitisha mkutano mkuu wa marekebisho ya katiba ndani ya siku 40 kuanzia jana (kabla ya Aprili 15, 2013).
Katika agizo la tatu, serikali imeitaka TFF iitishe mkutano mkuu kwa kuzingatia katiba ya mwaka 2006 na kwamba, kwenye mkutano huo wajumbe wapitishe marekebisho yaliyofanywa hadi mwaka 2008.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikaririwa akisema jana kuwa hawezi kuzungumzia lolote kuhusiana na matokeo ya kikao chao cha jana na serikali kwa sababu mwenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo ni Rais wa TFF, Leodger Tenga ambaye hakuwapo nchini.
Maagizo hayo ya serikali yametolewa katika kipindi ambacho tayari serikali imeshatangaza kuifuta katiba mpya ya TFF (ya mwaka 2012) na kuamuru itumike ya 2006, bila kujali ahadi ya FIFA kutuma ujumbe wake katikati ya mwezi huu kujaribu kutatua mgogoro wa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo.
Hata hivyo, kwa mujibu katiba ya TFF ambayo inazingatia maelekezo ya FIFA, ibara ya 25(1) na (2), mwenye mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu wa TFF ni kamati ya utendaji ya shirikisho hilo au theluthi mbili ya wajumbe wa mkutano mkuu ambao hutakiwa kuomba kuitishwa mkutano mkuu kwa maandishi.
Katiba hiyo ya TFF haitoi nafasi kwa serikali kuamuru kuitishwa mkutano mkuu.

Rais wa TFF, Leodger Tenga

HATARI YA KUFUNGIWA
Ingawa hadi kufika jana haikufahamika kama TFF watatekeleza maagizo hayo ya serikali,
lakini uzoefu katika maeneo mengine unaonyesha kuwa utekelezaji wa amri hiyo utaiweka Tanzania katika hatari kubwa ya kufungiwa na FIFA ambayo inapinga vikali serikali kuingilia masuala ya soka.
Novemba 2006, Kenya ilifungiwa na FIFA kutokana na serikali kuingilia masuala ya soka na kushindwa kufuata taratibu za chombo hicho cha kusimamia mchezo wa soka duniani.
FIFA waliiondolea Kenya kifungo hicho Machi 9, 2007 baada ya Waziri Kamanda 'kuinua mikono' kwa kutangaza hadharani kuwa kamwe hawataingilia tena masuala ya KFF kufuatia 'mashinikizo' makubwa kutoka ndani na nje ya taifa hilo.
Ujumbe wa FIFA ulienda Kenya kutoa mwongozo wa kurejesha soka la Kenya katika hali ya kawaida ikiwamo kumtaka waziri wa michezo akiri kutoingilia tena uendeshaji wa KFF.
Rais wa Nigeria, Jonathan Goodluck aliamuru nchi yake isishiriki tena michuano yoyote ya soka ya kimataifa kwa nia ya kujipanga upya baada ya timu yao ya taifa ya soka kuondoshwa kwa aibu kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.
Hata hivyo, ilifahamika baadaye kuwa maamuzi hayo ya rais yalikuwa na nia ya kumdhibiti mmoja wa viongozi wa juu wa shirikisho la soka la nchi hiyo (NFF), Amos Adam aliyekuwa mbioni kuwania tena uongozi.
Kutokana na kitendo hicho cha serikali kuingilia soka, FIFA iliipa serikali ya Nigeria saa 48 kufuta agizo lake na kwamba, vinginevyo ingefungiwa. Saa chache baadaye, serikali ya Nigeria ilisalimu amri kwa kutangaza kufuta agizo lake baada ya rais Jonathan kuteta ikulu na Adam.

MGOGORO TFF
Chanzo cha mgogoro wa uchaguzi wa TFF ni kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea, wakiwamo Jamal Malinzi anayewania kugombea urais na Michael Wambura anayeutaka umakamu wa rais.

No comments:

Post a Comment