HII NDIYO HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI ILIYOLETA VURUMAI JANA
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE.
EZEKIAH DIBOGO WENJE (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni katika bajeti ya wizara hii mwaka 2012/13, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ilibaini mapungufu mengi ya kiutendaji
na kiuwajibikaji katika wizara hii, na hivyo kuitaka Serikali kufanya mambo
yafuatayo ili kuboresha utendaji na ufanisi:
1. Kuziwezesha balozi zetu nje kwa kuzitengea fedha za kutosha
ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi
2. Kutoa idadi ya majengo ya balozi zetu nje (nyumba za
mabalozi, nyumba za maafisa wa balozi na ofisi za balozi) kwa mchanganuo wa
idadi ya nyumba katika nchi na kama nyumba hizo zina hati miliki au la.
3. Kutoa taarifa ya namna kila ubalozi ulivyotekeleza sera ya
Diplomasia ya uchumi kwa kuzingatia kwamba balozi nyingi ziko hoi kifedha kiasi
cha kwamba waambata wa kiuchumi wanakosa fedha za kusafiri kutoka sehemu moja
hadi nyingine kwa ajili ya upelelezi wa masuala ya kiuchumi.
4. Kulikarabati jengo la ubalozi wa Tanzania huko Msumbiji
lililokuwa limechakaa kwa kutofanyiwa ukarabati tangu 1975 ingawa jengo hilo
tulipewa bure na Serikali ya Msumbiji chini ya FRELIMO.
5. Kujenga kitega uchumi katika kiwanja cha Tanzania
kilichopo Dubai na kukiendeleza kiwanja namba 19 tulichopewa bure na Serikali
ya Uingereza kilichopo Uingereza (Central London) ambavyo vimekuwa maficho ya
wezi kwa kutoendelezwa kwa muda mrefu na kusababisha Serikali za nchi hizo
kutaka kutaifisha viwanja hivyo.
6. Kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za balozi zetu nchini China,
na Uingereza kutoa hati za kusafiria kwa mataifa mengine hasa ya Afrika
Magharibi ili kubaini ukweli na kuliondolea taifa aibu kutokana na tuhuma hizi.
7. Kukarabati jengo la ubalozi wetu nchini China ambalo lilikuwa
na nyufa na kuvuja nyakati za mvua, na kununua samani na vifaa vya ofisi
kama mashine za nukushi na za kurudufu ambazo zilikuwa hazipo,
8. Kununua magari mapya ya ofisi ya ubalozi wetu nchini China
kwa kuwa magari matatu yaliyokuwepoyalikuwa yameshapitiliza muda wa miaka
10 ambao kwa mujibu wa sheria za China hayapaswi kutumika tena,
9. Kupeleka mwambata wa kiuchumi (economic attaché) nchini
China ili kufuatilia fursa mbalimbali za kiuchumi katika kutekeleza diplomasia
ya uchumi kutokana na mahusiano makubwa ya kibiashara kati ya nchi yetu
na China
10. Kuwawekea zuio wahusika wa kashfa ya rada kuwa viongozi wa
shughuli za kiserekali ili walau kuonesha uwajibikaji wa kimaadili (moral
accountability) baada ya kushindwa kuwawajibisha kisheria, ili kuondoa dhana
iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba dola imetekwa na mafisadi.
11. Kuchunguza na kuwachukulia hatua watanzania (wafanyabiashara
na wanasiasa) waliotorosha kiasi kikubwa cha fedha za nchi yetu (zaidi ya
shilingi bilioni 315) na kuzificha katika mabenki ya uswisi
12. Kutoa mchanganuo wa jinsi fedha za rushwa ya rada (chenji ya
rada) zilivyotumika
13. Kueleza bayana faida za kiuchumi tunazopata kama taifa kwa
kushirikiana na jumuiya mbalimbali za kimataifa ili kuthibitisha kwamba
mashirikiano hayo hayatumiki kupora rasilimali za nchi yetu kwa hila ya
“uwekezaji”
Mheshimiwa Spika, kabla sijajielekeza kwenye mambo mahsusi kwa
kipindi hiki cha bajeti ya 2013/2014, napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kuitaka Serikali kutoa
majibu mbele ya Bunge hili tukufu, kwamba imetekeleza kwa kiwango gani masuala
yaliyoorodheshwa hapo juu, tuliyoitaka iyatekeleze (moja baada ya jingine) kwa
mwaka wa fedha unaomalizika wa 2012/2013?
1.1 Upotevu wa Fedha za Safari za Rais, Shilingi bilioni 3.5
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2012/2013
nilihoji kuhusu serikali Kuchunguza na kuchukua hatua kwa waliohusika na
upotevu wa shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya safari “hewa” za Rais nje ya nchi,
ili waweze kubainika na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni nyingi sana na hasa
ikikukumbukwa kuwa mwaka jana 2012 wapo mawaziri ambao walichukuliwa
hatua na Bunge hili kutokana na upotevu ama madhaifu yaliyofanyika kwenye
wizara zao, wapo ambao walihukumiwa kutokana na kupotea kwa Twiga kwenye wizara
zao, wapo waliohukumiwa kutokana na udhaifu katika kusimamia wizara zao na
taasisi zilizoko chini yao.
Kambi rasmi ya upinzani, inahoji iweje leo waziri aliyeshindwa
kusimamia wizara yake na kusababisha upotevu wa fedha hizi mpaka leo bado yupo,
wakati wapo mawaziri wengine walioshughulikiwa kutokana na udhaifu walioonyesha
kwenye kusimamia wizara zao, au ndio kusema kuwa Serikali hii ya CCM inafanya
upendeleo na kuonea baadhi ya mawaziri na kuwaacha wengine? “This clearly
indicates the “double standard” nature of this Government in the performance of
its functions”
1.2. Kuanzishwa kwa Ubalozi Mdogo Guangzhou -China
Mheshimiwa Spika, mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilipendekeza kuwa serikali ianzishe ubalozi mdogo katika Jiji la Guangzhou kwa
ajili ya kurahisisha biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa
China. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inatambua kuwa serikali imelifanyia
kazi wazo hili na imeamua kuanzisha ubalozi mdogo katika mji huo ,ila tunataka
kujua ni lini ubalozi huu utazinduliwa rasmi, kupata watendaji na vitendea kazi
ili uweze kuanza kufanya kazi .
2.0 DIPLOMASIA YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, moja ya matarajio ya ushirikiano wa kimataifa
ni kuweza kutafuta, na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza
kupatikana katika mashirikiano hayo ili kama Taifa, tuweze kujikwamua kiuchumi
na kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, kinyume na matarajio hayo mazuri, sasa nchi
yetu imegeuzwa kuwa kitega uchumi cha nchi zilizoendelea kwa kisingizio cha
“ushirikiano wa kimataifa” chini ya mwavuli wa “uwekezaji”. Matokeo ya
ushirikiano huu wa kinyonyaji (exploitative relationship) ni kwamba kiwango cha
umasikini katika nchi yetu kimeongezeka na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa
tegemezi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla.
Mheshimiwa Spika, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alikerwa na unyonyaji na unyanyasaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni, hali
iliyompelekea kusema maneno yafuatayo:
“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha,
tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndiyo uliotufanya tuonewe, tunyonywe
na kupuuzwa. Sasa tunataka kufanya mapinduzi”
Mheshimiwa Spika, baada uhuru, Mwalimu akaanzisha siasa ya
Ujamaa na Kujitegemea. Ujamaa ulilenga kujenga umoja wa kitaifa na umoja
wa bara la Afrika dhidi ya unyonyaji wa kibeberu, wakati kujitegemea
kulimaanisha kujenga uchumi endelevu ili kulijengea taifa heshima na
nguvu ya maamuzi mbele ya mataifa mengine, na kuliepusha taifa na fedheha ya
kuombaomba.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa
sana na kitendo cha Serikali kulidanganya taifa, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya 2010 kwamba: “Katika kipindi cha miaka mitano 2010 -2015, Serikali ya
Chama cha Mapinduzi itatekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi” wakati Ibara ya
98 (i) ya Ilani hiyohiyo ya CCM inasema kwamba Serikali ya CCM itaendelea
kushinikiza nchi tajiri kutekeleza ahadi yao ya kutenga asilimia 0.7 ya pato la
taifa la nchi zao kwa ajili ya misaada kwa nchi masikini”.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba ahadi hii ya asilimia 0.7 ya
pato la taifa la nchi tajiri ambayo Serikali ya CCM inakodolea macho ni fedha
za walipa kodi wa nchi hizo kama ambavyo wananchi wetu wanavyolipa kodi. Aidha
ni aibu kwa Serikali hii ya CCM kuchukua ahadi za wahisani na kuziweka kwenye
ilani ya uchaguzi ya CCM kama ahadi kwa wananchi ili kubembelezea kura.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uvivu wa kufikiri na kubuni mbinu
za kuikwamua nchi hii na umasikini, Serikali hii ya CCM sasa hivi imeachana
kabisa na sera ya kujitegemea, ambayo Mwalimu kupitia Azimio la Arusha alisema
kwamba “ … Hakika ni ujinga na upumbavu zaidi kwetu sisi, kufikiri kwamba
tutaondokana na umasikini wetu kwa misaada ya fedha kutoka nje kuliko
rasilimali zetu wenyewe”
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kulieleza bunge hili, kama inatekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutegemea ahadi
ya misaada ya fedha kutoka kwa wahisani na kama hilo ndio suluhisho la matatizo
yanayokumba uchumi wetu kama taifa kwamba tutaweza kuendelea kwa kutegemea
hisani na fadhila za wafadhili huku tukishindwa kuzitumia rasilimali zetu kwa
ajili ya kujikomboa kiuchumi.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani imejiridhisha kwamba kauli mbiu
ya ‘Diplomasia ya Uchumi’ imeendelea kubakia kama ilivyo kauli mbiu ya
‘Kilimo Kwanza’ ambayo imebakia kutamkwa na viongozi bila kuwa na mkakati wa
utekelezaji wala vigezo vya kupima kiwango cha utekelezaji wake.
3.0. VYAMA VYA SIASA NA MISAADA KUTOKA NJE YA NCHI.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa
Mataifa ‘United Nations University’(UNU-WIDER) ya mwezi Aprili 2012
iliyoandaliwa na Aili Mari Tripp ilionyesha kuwa misaada ya wahisani kutoka nje
katika mabadiliko ya kisiasa Tanzania ‘Donor Assistance and Political Reform in
Tanzania’, inaonyesha kuwa Tanzania imepokea misaada kutoka nje yenye thamani
ya dola za kimarekani bilioni 26.85 toka mwaka 1990-2010.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa Tanzania ni
nchi inayoongoza kusini mwa jangwa la Sahara kwa kupokea misaada mingi kutoka
nje ya nchi na hasa kutoka mataifa ya Ulaya na taasisi za nchi za Uingereza,
Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Canada, Sweden, na taasisi kama Benki ya
Dunia, IMF ,UNDP ,UNICEF na mengineyo.
Pamoja na misaada yote hiyo, bado tumeendelea kuwa nchi maskini
sana duniani pamoja na kuwa na rasilimali lukuki ambazo tumepewa na Mungu ila
tunashindwa kuzitumia kwa manufaa ya watanzania na badala yake tumeendelea
kudanganywa na vimisaada vidogo vidogo na kubadilishana na rasilimali zetu kama
madini, misitu ,wanyama nk kwa ajili ya misaada hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na misaada hiyo kwa serikali hii ya CCM
bado vyama vya siasa vimekuwa na mahusiano na baadhi ya vyama vingine vya siasa
katika mataifa ya magharibi na vimekuwa vikipokea misaada ya aina mbalimbali
kama fedha , nyenzo na mengineyo kadiri ya makubaliano na mirengo ya kiitikadi
ya vyama husika.Pamoja na ukweli huo bado vipo vyama vya siasa vinavyopotosha
umma kuhusiana na misaada vinayopokea kutoka nje ya nchi na vyama hivi vimekuwa
mstari wa mbele kueneza propaganda za uongo kuwa vyenyewe havipokei misaada
kutoka nchi za magharibi.
Mheshimiwa Spika, CCM wao ‘wanajiita’ kuwa wapo mrengo wa
kijamaa/kikomunisti na wamekuwa wakipokea misaada mingi sana ya fedha na nyenzo
kutoka Umoja wa Vyama vya Kikomunisti Ulimwenguni ‘Socialist International’
kutoka katika nchi kama za Ujerumani kupitia SDP ,Uingereza kupitia chama cha
Labour,China kupitia chama cha Kikomunist ,Marekani kupitia chama cha
Democrats. Pamoja na misaada ya kifedha na kiufundi ambayo CCM imekuwa ikipata
kutoka nje wamekuwa hawatangazi hadharani hata mara moja kuhusiana na kiasi
ambacho wamekuwa wakipokea na hivyo kila kitu kwao imekuwa ni siri kuu ya
viongozi wao.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa chama cha CUF, kutokana na
itikadi zake za mrengo wa Kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni
pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga”. Hii ni
kwa mujibu wa tangazo lao kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali
ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn
Featherstone kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho([url]www.liberal-international.org[/url])
kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki
ya mtu mmoja mmoja, wanashirikiana na vyama kama vile LPC ya Canada, Det
Radikale Venstre cha Norway, FDP cha Ujerumani, Israel Liberal Group cha
Israel,PDS cha Senegal na Liberal Democrats cha Uingereza.
Kutokana na umoja huo, CUF wamekuwa wakipata msaada wa kifedha
na nyenzo nyingine mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vya mrengo wa Kiliberali
na msaada wa mwisho ni hivi majuzi mwezi Machi 2013 waliposaini makubaliano na
chama cha Kiliberali kutoka Norway.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa CHADEMA, wapo kwenye Umoja wa
Vyama vya Kidemokrasia Ulimwenguni (International Democratic Union - IDU). Huu
ni umoja wa vyama ambavyo vipo kwenye mrengo wa kati na ambavyo msingi wake
mkuu ni pamoja na kuwa na familia, kama taasisi muhimu katika jamii,
ikimaanisha kwamba: “tunapinga vitendo vyote vya ushoga na usagaji”. Tunatetea
demokrasia, haki za binadamu na kupambana na ufisadi katika serikali. Vyama
wanachama wa umoja huu ni pamoja na Conservative Party cha UK, CPP cha Norway,
Republican cha Marekani na vingine vinavyofuata mrengo huo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inavitaka vyama
vyote ambavyo vimekuwa na mahusiano na vyama vya nje viweke wazi mikataba yao
na malengo ya mahusiano hayo ikiwa ni pamoja na misaada ambayo vimekuwa
vikipokea kutoka kwenye nchi hizo .
4.0 MPANGO WA KUJITATHIMINI KIUTAWALA BORA (APRM)
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Januari, 2013
ulifanyika mkutano wa 20 wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mjini
Addis Ababa ,Ethiopia na ni katika mkutano huo Mhe. Rais Kikwete aliwasilisha
taarifa ya nchi yetu kuhusu kujitathimini katika utawala bora kwenye mpango wa
nchi zinazojitathimini katika utawala bora (APRM).
Mheshimiwa Spika, baada ya taarifa hiyo (randama uk.15) nchi
yetu ilitakiwa kutafutia ufumbuzi changamoto zifuatazo;
i. Migogoro baina ya wakulima na wafugaji
ii. Imani za kishirikiana (uchawi)
iii. Kuhakikisha kuwa manufaa ya kukua kwa uchumi yanawafikia
wananchi
iv. Kutoa elimu kwa umma kuhusu mipango na sera za serikali
Mheshimiwa Spika, changamoto hizi ambazo nyingine zinatia aibu
taifa letu mbele ya mataifa mengine kama vile sisi kuonekana ni wachawi na
hivyo kutakiwa kuchukua hatua dhidi ya uchawi !ni fedheha na aibu kubwa kwa
taifa letu .
Aidha , Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inataka kujua serikali
na wizara imechukua hatua gani mpaka sasa katika kukabiliana na changamoto hizi
na hasa tatizo la wakulima na wafugaji na kuhakikisha kuwa manufaa ya kukua kwa
uchumi wetu yanawanufaisha wananchi na sio kuwanufaisha baadhi ya viongozi na
mafisadi wachache.
5.0 MLIPUKO WA BOMU ARUSHA NA BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA
MATAIFA.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu tarehe 05 Mei, Kanisa
Katoliki Parokia ya Olasiti huko Arusha lililipuliwa kwa bomu.
Tukio hili lilitokea wakati akiwepo balozi wa Vatican Nchini na ambaye
ndio alikuwa mgeni wa heshima kwenye tukio la kuzindua Parokia hiyo.
Mheshimiwa Spika, mara baada ya tukio hilo, Balozi wa Vatican
nchini aliwasilisha taarifa hiyo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
na kuonyesha kuwa Tanzania sio nchi salama sana kutembelewa na wageni na kama
wakitembelea basi wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa kwa kipindi chote
watakapokuwa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua
nini kauli ya serikali kuhusiana na tukio hili na hasa kuhusiana na taarifa za
hali ya usalama wa nchi yetu na wageni zilizowasilishwa kwenye Baraza la
usalama la Umoja wa Mataifa .
6.0 SAFARI ZA VIONGOZI NJE NA MISAFARA MIKUBWA
Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2011/2012 Kambi rasmi ya Upinzani
Bungeni imekuwa ikihoji suala la misafara ya Viongozi wa kitaifa kuwa mikubwa
kutokana na kuambatana na watu wengi ambao wengine wanakuwa hawana hata
majukumu ya msingi ya kufanya wakati wa ziara hizo huku wakiliongezea taifa
gharama kubwa ya kuwasafirisha na na kulipia malazi yao na starehe zao.
Aidha , tumekuwa tukipendekeza na kushauri kuwa sasa ni wakati
muafaka kwa Rais wa nchi kuamua kutuma wasaidizi wake kwenye baadhi ya ziara za
nje kama wanavyofanya viongozi wengine wa nchi jirani kama Rais Kagame wa
Rwanda na hata Mwai Kibaki, Rais mstaafu wa Kenya alivyokuwa anafanya
akiwa Rais, kwani kwa kufanya hivyo atapunguza msururu wa maafisa na viongozi
mbalimbali wa kuambatana naye. Tunashauri tena kuwa rais awe anatuma wasaidizi
wake kwenye ziara za kawaida na yeye awe na jukumu la kushiriki kwenye ziara
rasmi za kiserikali ‘State Visits’ na mikutano maalum ya Kimataifa kama UN na
AU.
Hivyo basi Kambi rasmi ya Upinzani inashauri mambo yafuatayo
yafanyike ili kupunguza gharama hizi kubwa za kuwasafirisha viongozi na
misafara isiyokuwa na tija kama ifuatavyo;
i. Serikali itengeneze kanuni za kuthibiti idadi ya maafisa na
watu ambao watakuwa wakiambatana na Rais kwenye ziara za nje (idadi ya wajumbe
kwenye misafara iwe wazi na ijulikane)
ii. Pawepo na kanuni za kuainisha kuwa ni nani watapaswa kupanda
ndege daraja la kwanza na wale wenye haki ya kulala kwenye hoteli za daraja la
kwanza wajulikane.
6.1. Idara ya Protocol na Mabilioni ya Fedha za Safari za Nje.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 fungu 221100
‘travel out of country’zilitumika shilingi 36,121,942,870.00 kwa ajili ya
safari za nje ya nchi kwa viongozi wakuu. Katika mwaka wa fedha uliopita wa
2012/2013 kifungu 1010 ambacho ni kwa ajili ya protocol walitengewa shilingi
8,372,581,824 na fedha ambazo zilikuwa zimepokelewa na wizara mpaka mwezi
Februari 2013 zilikuwa jumla ya shilingi 26,081,860,727.16! (randama
uk.4)jedwali la 2 na zilitumika kwa ajili ya kugharamia safari za viongozi nje
ya nchi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 Bunge lilikuwa
limetenga na kuidhinisha kiasi cha shilingi 8,372,581,824 kwa ajili ya kifungu
hiki cha Protocol ‘travel out of Country’kwa mujibu wa kitabu cha matumizi ya
kawaida juzuu ya pili (volume II). Jambo la kushangaza ni kwamba, wizara
iliieleza kamati na Bunge hili kuwa walishatumia zaidi ya bilioni 26.081 kutokana
na fedha walizokuwa wamejitengea wenyewe wizara ambazo hazikuidhinishwa na
Bunge kiasi cha bilioni 29.404
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa
na CHADEMA, inataka maelezo ya kina kuhusiana na mamlaka ya wizara hii kwenda
kutenga na kutumia fedha nyingi kuliko zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili
na zilikuwa fedha kwa ajili ya safari za kwenda nje ya nchi, ni nani aliipa
wizara mamlaka hiyo na kiburi hicho kiasi cha kupuuza maamuzi ya Bunge hili
tukufu.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kitengo
hiki cha Protocol kimetengewa jumla ya shilingi 15,155,377,400.00 kwa ajili ya
matumizi mengineyo ,ambazo katika mchanganuo wake kwenye kifungu 1010 kifungu
kidogo cha 221100 ‘travel out of Country’ zimetengwa shilingi 9,381,328,850.00
kwa ajili ya kugharamia safari za kikazi za viongozi wa Kitaifa nje ya nchi.
Aidha, katika kifungu kidogo cha 220700 ‘rental expenses’
zimeombwa jumla ya shilingi 2,925,445,000.00 kwa ajili ya kukodisha ndege
,magari na kumbi za mikutano kwa ajili ya viongozi wa kitaifa.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, haikubaliani na kamwe
haitakubaliana na ufujaji huu wa fedha za walipakodi maskini wa Tanzania .
Tunamtaka waziri atoe maelezo ya kina kwa watanzania ni kwanini nchi maskini
kama yetu tutumie fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya safari za viongozi nje
ya nchi? Aidha , hatukubaliani na kitendo cha kutenga fedha kwa ajili ya kukodi
ndege wakati Rais ana ndege yake ambayo ilinunuliwa na mabilioni ya
fedha za watanzania.
Ikumbukwe kwamba ndege hii ya Rais ilinunuliwa kwa mbwembwe
nyingi kiasi kwamba Waziri wa Fedha wa wakati huo Ndugu Bazili Mramba alisema
watanzania wafunge mkanda, hata kama watakula majani, lazima ndege ya Rais
inunuliwe. Watanzania hawa wamekula majani sasa kiasi cha kutosha, bado tena
Serikali inaendelea kuwanyonya ili ipate pesa za kukodisha ndege wakati Rais
ana ndege? Hivi Serikali sasa inataka watanzania wale mawe ndio ijue kwamba
watu wamefunga mkanda kiasi cha kutosha?
6.2 Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo
ya Nje Ulinzi na Usalama, ilifanya ziara kwenye balozi takribani zote na iliona
matatizo yanayozikumba balozi zetu huko na ilikuwa matumaini yetu kuwa baada,
ya ziara ile ya kamati ingehakikisha kuwa fedha zinaongezwa kwenye wizara hii
na hasa kwenye fungu la maendeleo ili tuweze kuboresha mazingira ya balozi
zetu. Kinyume na matumaini hayo, ni kwamba hakuna jitihada zilizofanyika
kuongoeza bajeti ya wizara hasa katika fedha za maeendeleo.
Mheshimimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka
kamati ya Bunge ya Ulinzi na usalama, kuishinikiza Serikali ili kuhakikisha
kuwa katika mwaka huu wa fedha wizara hii inaongezewa fedha kwa ajili ya
kuboresha mazingira ya balozi zetu , na hiyo ndio njia pekee ya kuonyesha kuwa
kamati haikuenda kufanya utalii bali ilienda kuona matatizo ya balozi zetu na
kuchukua hatua.
7.0 UFISADI KATIKA UNUNUZI WA JENGO LA OFISI NA MAKAZI KATIKA
UBALOZI WA TANZANIA JIJINI PARIS – UFARANSA.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha kwa mujibu wa
randama ya wizara ni kuwa mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 28
(28,000,000,000.00) zimepangwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na kati ya
hizo kiasi cha shilingi bilioni 24 na milioni 188 (24,188,000,000.00) ni kwa ajili
ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi ya balozi jijini Paris ,Ufaransa
(randama uk 25) na kiasi cha shilingi bilioni 3 na milioni 812
(3,812,000,000.00) ni kwa ajili ya gharama za ukarabati wa majengo ya ofisi na
makazi yaliyopo Ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, ukisoma randama ya wizara (uk.120) katika
kasma 6391 ,kifungu kidogo 411100 kiasi cha fedha kilichoombwa ni shilingi
bilioni 23 na milioni 900 (23,900,000,000) kwa ajili ya ununuzi wa jengo la
ofisi na makazi ya Balozi jijini Paris, Ufaransa na shilingi bilioni 3
namilioni 700 (3,700,000,000.00) kinaombwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya
ofisi na makazi yaliyopo ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji.
Hata hivyo, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kwenye kasma
6391 katika fungu la Maendeleo (randama uk.120) wizara inaomba kutengewa kiasi
cha shilingi milioni 400 (400,000,000.00) (kifungu 221100 ) fedha ambazo hazipo
kwenye kitabu cha matumizi ya kawaida juzuu ya pili (volume II) kwa ajili ya
posho ya kujikimu na gharama za usafiri kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa
miradi ya maendeleo ya Wizara, miradi yenyewe ni miwili mmoja wa kununua nyumba
Ufaransa na kukarabati jengo Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, mkanganyiko huu wa kimahesabu unatia mashaka
makubwa sana kuhusiana na dhamira ya serikali na wizara hii hasa fedha
zinapotengwa bila kufuata utaratibu wa kibajeti na bila kuingizwa kwenye vitabu
vya fedha na mafungu husika.
Kambi rasmi ya Upinzani, inajiuliza tunapitisha mafungu yapi?
Kwani kwenye randama fedha zinatofautiana kwenye fungu moja la maendeleo baina
ya (ukurasa 25 na 120) , vilevile kwenye kitabu cha matumizi ya kawaida hali ni
tofauti kwenye fungu la travel out of the Country kwani sasa wizara
imejiongezea shilingi milioni mia nne kwa ajili ya kufuatilia miradi miwili
ambayo ni kununua jengo Paris na kukarabati Jengo la ubalozi - Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, utata wa fedha unaendelea kuonekana kwenye
randama ya wizara katika kiambatanisho Na.1 ‘utekelezaji wa ushauri na
mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge ya mambo ya nje na ushirikiano wa
kimataifa’ katika ushauri/mapendekezo Na.5 kamati iliitaka ‘Wizara itoe
mchanganuo wa matumizi ya fedha za bajeti ya maendeleo zilizopokelewa kutoka
hazina katika mwaka wa fedha 2012/13’
Maelezo ya wizara yalikuwa kama ifuatavyo; nanukuu randama ya
wizara “katika mwaka wa fedha 2012/2013 ,hadi kufikia mwezi Machi ,2013 wizara
imepokea kutoka Hazina kiasi cha shilingi 13,261,281,600.00 ambapo kati ya
fedha hizo kiasi cha shilingi 9,660,000,000.00 zimetumika kwa ajili ya kulipia
malipo ya awali ya ununuzi wa Jengo la Ofisi na Makazi ya Balozi
Paris,Ufaransa;shilingi 995,930,000.00 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa
jengo la serikali lililopo Maputo,Msumbiji ;shilingi 626,899,155.00 zimetumika
kwa ajili ya ukomboaji wa vifaa vya ujenzi bandarini vilivyotumika katika
ujenzi wa kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere na safari ya
kikazi ya wataalam katika balozi za Maputo,Pretoria na Lusaka kwa ajili ya kazi
ya upembuzi yakinifu wa miradi ya maendeleo iliyopo katika Balozi hizo; na
shilingi 1,978,452,485.20 bado hazijatumika na zinatarajiwa kutumika kwa ajili
ya kulipia gharama za ukarabati wa jengo la Serikali lililopo Maputo’
Mheshimiwa Spika, baada ya kufuatilia na kufanya tathimini ya
kina kuhusiana na majibu hayo ya wizara kuhusu fedha za maendeleo kwa ajili ya
ukarabati wa Jengo la Maputo na kununua Jengo la Ofisi na Makazi ya Balozi
Ufaransa na kukuta kuwa ni fedha nyingi sana kuliko uhalisia wenyewe , kwa
mfano waziri anataka Bunge na taifa tuamini kuwa kufanya ukarabati wa jengo
moja la ofisi Maputo Msumbiji tunahitaji kutumia kiasi cha shilingi
4,695,930,000.00 kwa kutumia fedha inayoombwa mwaka huu wa fedha na zile ambazo
tayari zilishalipwa katika mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Aidha wakati wizara inawasilisha majibu yake kwenye kamati ya
kudumu ya Bunge walisema kuwa (swali 12 uk.5) ‘kiasi cha fedha kilichotengwa
kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Serikali yaliyopo Maputo ni shilingi
3,812,000,000.00……kiasi hicho cha fedha kinatosheleza kukamilisha kazi ya
ukarabati wa majengo hayo ya Serikali yaliyopo Maputo, Msumbiji’
Aidha, kununua jengo moja la ofisi na makazi katika Jiji la
Paris Ufaransa tunahitaji kutumia kiasi cha shilingi bilioni 33 na milioni 560
33,560,000,000.00.
Mheshimiwa Spika, kwa majibu haya ya wizara ni kuwa tayari
wizara imeshafanya malipo ya shilingi bilioni 9.66 kama malipo ya awali kwa
ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi huko Paris Ufaransa , na kuwa
tayari tumeshafanya malipo ya awali kiasi cha shilingi milioni 995.930 kwa
ajili ya ukarabati wa jengo la ubalozi huko Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, hakika kiasi hiki ni kikubwa kupitiliza na
hata utafiti na tathimini ambayo ilifanywa na Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni
ilionyesha kuwa kununua jengo la ofisi katika jiji la Paris kwenye mji wa bei
ghali kama Co’te d’Azur (most expensive area in Paris) huwezi kutumia fedha
nyingi kiasi hicho kwa ajili ya manunuzi ya jengo la ofisi na makazi.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunakumbuka sakata la
ununuzi wa jengo la ubalozi lililomkumba balozi Prof.Mahalu huko Roma - Italia
na yaliyofuatia mpaka kesi na fedha zetu tulizoambiwa kuwa zimepotea hazikuweza
kurejeshwa baada ya Prof.Mahalu kushinda kesi hiyo mahakamani.
Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata
majibu kuhusiana na mambo yafuatayo;
i. Ni eneo gani ambalo tumepata jengo la kununua kwa ajili ya
ubalozi na makazi ya balozi huko Paris, Ufaransa, na ni nyumba ya aina gani .
ii. Je, Serikali inaweza kuonyesha mkataba wa manunuzi wa nyumba
hizo (Paris) kwa Bunge na tutalipa kiasi gani kununua jengo hilo?
iii. Ni nani au wakala gani wa serikali aliyefanya tathimini ya
hayo majengo na kuamua kuwa tulipe kiasi hicho cha fedha?
iv. Ni kampuni gani iliyohusika katika kufanya makubaliano ya
mauziano ya nyumba hizo na tunawalipa kamisheni ya shilingi ngapi?
v. Nani, aliidhinisha kutumika kwa kiasi kikubwa hivyo kwa ajili
ya kununua jengo la Ubalozi na makazi huko Paris, je Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Mambo ya Nje, ilishirikishwa katika manunuzi haya?
vi. Ukarabati unaofanywa kwenye jengo la Maputo Msumbiji ni wa
aina gani, au tunajenga upya nyumba hizo?
vii. Ni kampuni gani ya ujenzi inayofanya ukarabati wa jengo
letu huko Msumbiji na mkataba wa ukarabati huo uko wapi, tungetaka uwekwe
hadharani.
Aidha , kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , inatoa hoja ya kumtaka
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi maalum
(Special Audit) kuhusiana na ununuzi wa majengo haya na ukarabati unaofanyika
kwenye jengo letu huko Maputo, Msumbiji, na kuona kama thamani halisi ya fedha
imezingatiwa , na kama sheria ya manunuzi ya umma imefuatwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Vile vile, tungetaka sehemu ya fedha hizi
zitumike kwa ajili ya kukarabati jengo letu la zamani la ubalozi lililopo Washngton
ambalo kwa sasa halitumiki baada ya kutekelezwa kwani likikarabatiwa litaweza
kuliongezea taifa mapato kutokana na matumizi ya kibiashara ya jengo hilo.
8.0 MPANGO WA WIZARA WA KUTOA VISA KWENYE BALOZI TU
Mheshimiwa Spika, mpango wa Wizara kutoa visa kwenye balozi tu
haukubaliki. Kwa Mujibu wa majibu ya wizara kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya
Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ilionyesha kuwa ili wizara iweze
kukusanya fedha za kutosha kwenye balozi zetu ni kwa kurudisha utaratibu wa
utoaji wa viza kufanywa na Balozi zetu tofauti na utaratibu unaotumika hivi
sasa ambapo wageni huweza kupatiwa viza pindi wanapowasili katika vituo vya
kuingilia nchini (viza on arrival).
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, haikubaliani na wazo hili la
wizara kwani badala ya kuongeza wageni kuja nchini litapunguza sana hasa
ikizingatiwa kuwa ni nchi chache sana ambako tuna ofisi za Balozi na pia kuna
nchi nyingine kama Marekani ambapo, kama mgeni yupo Carlifonia na anataka
kusafiri kuja Tanzania atalazimika kwanza kusafiri kwenda Washington ambako
ndiko kwenye ubalozi atafute visa na ndipo aweze kuja nchini. Utaratibu
huu utaongeza gharama kubwa za usafiri kwa wageni na watalii na hivyo
kulipotezea taifa mapato yataokanayo na utalii kwani wageni watapungua.
Aidha, tunaikumbusha wizara kuhusiana na Itifaki ya kuwa
na“Single Tourist Destination Protocol” na uwepo wa hati ya kusafiria na visa
moja ya utalii “Single Tourist Visas” kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, hivyo kama sisi tukifanya huo uamuzi basi wenzetu Kenya wataendelea
kupata wageni wengi zaidi kutokana na visa ya pamoja na wageni wataingia
Tanzania kutokana na visa za Kenya chini ya Itifaki hiyo.
8.1 Mkutano wa Mabalozi wa Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa Spika, wizara inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 1
kwa ajili ya kufanikisha mkutano wa mabalozi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 , na
wizara iliwasilisha maombi ya fedha hizo Hazina kama sehemu ya kipaumbele
lakini hazikuweza kupatikana .
Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inaitaka serikali kuiondoa aibu
hii na kutenga hizo fedha kwa ajili ya kufanikisha mkutano huo na tunapendekeza
kuwa katika fungu la protocol safari za nje ndipo fedha hizo zipunguzwe na
kutumika kwa ajili ya mkutano wa mabalozi wetu ili waweze kupeana ushauri na
uzoefu,ili kuboresha ufanisi wa majukumu yao.
8.2 Utaratibu wa Kupeleka Fedha kwenye Balozi
Mheshimiwa Spika, kutokana na utaratibu wa kupeleka fedha kwenye
balozi zetu kuwa na mlolongo mrefu wa kwanza kutoka Hazina na kupelekwa
Wizarani, ndipo wizara isambaze fedha hizo kwenye balozi zetu mbalimbali
umesababisha fedha kuchelewa kufikishwa kwa wakati kwenye balozi zetu na hivyo
kusababisha usumbufu mkubwa na ucheleweshaji wa kazi kwenye balozi zetu.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka serikali kubadilisha
utaratibu huu na hazina iwe inapeleka fedha hizo moja kwa moja kwenye balozi
husika badala ya kuzipitisha wizarani kama ilivyofanya kwenye fedha za
Halimashauri mbalimbali nchini ili kupunguza usumbufu huo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya kambi rasmi
ya Upinzani naomba kuwasilisha.
________________________________
Ezekiah Dibogo Wenje
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
No comments:
Post a Comment