STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 31, 2013

Yanga yamwagiwa manoti

Add caption

KAMPUNI ya bia Tanzania (TBL), jana iliwakabidhi mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam hundi ya Sh. milioni 25 ikiwa ni motisha ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo wa msimu uliomalizika wa mwaka 2012/ 2013.
Akizungumza jana jijini, meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema kwamba wanaipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa huo na wanaamini udhamini wao kwa klabu hiyo ndiyo umesaidia kupatikana kwa matunda ya ushindi.
Simba ambao pia wanadhaminiwa na Kilimanjaro wamekosa kitita cha Sh. milioni 15 msimu huu kutoka TBL kutokana na kumaliza katika nafasi ya tatu kama ilivyokuwa kwa Yanga mwaka jana.
Kavishe alisema kuwa anafahamu ubingwa huo wa Yanga umetokana na klabu kuwa na mikakati imara ya ushindi ambayo waliipanga kuanzia mwanzo wa msimu.
Alisema kuwa kiasi hicho cha fedha TBL walichokiweka baada ya kuwapatia vifaa vya mazoezi na jezi, waliamini itakuwa ni chachu kwao kupambana na kumaliza kwenye nafasi mbili za juu na kwa msimu huu Yanga walifanikiwa kutwaa ubingwa.
"Tunafurahi kuona matunda na ushirikiano wa udhamini wetu umefanikiwa, tunajua kwamba klabu hizi mbili za Simba na Yanga tunazodhamini zinashindana kila mwaka na msimu huu umekuwa ni wa Yanga," alisema Kavishe.
Aliwataka wahakikishe msimu ujao pia wanafanya vizuri katika ligi hiyo licha ya kuwapo kwa changamoto kubwa katika kuubakiza ubingwa huo wanaoushikilia kutoka kwa timu nyingine.
Katibu mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, aliwashukuru TBL kwa kutimiza ahadi yao waliyoiweka kwenye mkataba na kuongeza kwamba ubingwa wao ulipatikana baada ya kukubali kukosolewa kila walipokosea.
Mwalusako alisema kwamba waliyafanyia kazi maoni na ushauri na kujirekebisha pale walipokosea na hicho ndiyo siri ya wao kutwaa ubingwa.
Alisema katika kujiandaa na msimu ujao, kikosi chao kitaanza mazoezi Jumapili huku pia kocha mkuu, Ernie Brandts, akitarajiwa kurejea nchini siku hiyo hiyo kutoka kwao Uholanzi alikokwenda kwa ajili ya mapumziko ya wiki mbili.

No comments:

Post a Comment