Waziri wa Elimu na Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa aliyetangaza matokeo hayo leo |
Matokeo hayo mapya yalitangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Dk. Kawambwa alisema kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia tisa hadi 43.
Waziri Kawambwa alitangaza matokeo hayo mapya, ikiwa ni wiki chache tangu serikali iyafute matokeo ya mtihani huo yaliyoyatangazwa na waziri huo, Februari 18, mwaka huu na kuliagiza Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kuyaandaa upya.
Kwa mujibu wa matokeo hayo mapya, jumla ya watahiniwa waliopata daraja sifuri ni watahiniwa 210,846, wavulana wakiwa 104,259 na wasichana ni 106,587.
Mbali na kuwaokoa watahiniwa hao, matokeo hayo mapya, yanaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa waliopata daraja la kwanza wameongezeka kutoka watahiniwa 1,641 waliotangazwa Februari 18, hadi watahiniwa 3,242 waliotangazwa jana.
Kati ya watahiniwa hao, ambao jumla yao ni 3,242, wavulana ni 2,179 na wasichana 1,063.
Pia idadi ya watahiniwa waliopata daraja la pili imeongezeka kutoka watahiniwa 6,453 waliotangazwa Februari 18, mwaka huu, hadi watahiniwa 10,355 waliotangazwa jana.
Kati ya watahiniwa hao, ambao jumla yao ni 10,355, wavulana ni 7,267 na wasichana 3,088.
Vilevile, idadi ya watahiniwa waliopata daraja la tatu imeongezeka kutoka watahiniwa 15,426 waliotangazwa Februari 18, mwaka huu, hadi watahiniwa 21,752 waliotangazwa jana.
Kati ya watahiniwa hao, ambao jumla yao ni 21,752, wavulana ni 14,979 na wasichana ni 6,773.
Kadhalika, idadi ya watahiniwa waliopata daraja la nne imeongezeka kutoka watahiniwa 103,327 waliotangazwa Februari 18, mwaka huu, hadi watahiniwa 124,260 waliotangazwa jana.
Kati ya watahiniwa hao, ambao jumla yao ni 124,260, wavulana ni 74,433 na wasichana ni 49,827.
Alisema kuanzia sasa matokeo ya kidato cha nne hadi cha sita yatachakatwa kwa kutumia mfumo wa viwango vya aina moja ambao hutumika kuchakata matokeo kwa masomo yote bila kujali kiwango cha kufaulu kwa somo husika.
Serikali iliyabatilisha matokeo hayo baada ya Necta kutumia mfumo mpya wa viwango vya ufaulu ambao ulisababisha wanafunzi takribani asilimia 60 kufeli.
Matokeo hayo yalilalamikiwa sana na makundi mbalimbali ya jamii.
Aidha wanafunzi kadhaa walijinyonga kutokana na kupata matokeo mabaya ambayo hawakuyatarajia na kuilazimisha serikali kuunda tume ya kuchunguza sababu za kufeli.
Hata hivyo, kabla ya tume hiyo iliyoongozwa na Profesa Sifuni Mchome, kuwasilisha ripoti, Baraza la Mawaziri lilikutana na kuiamuru Necta kuyafuta na kuyaandaa upya kwa kutumia mfumo uliotumika mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment