STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 28, 2013

King Kibadeni atua rasmi Msimbazi na mikwara, Julio achekelea


Kocha Abdallah Kibadeni akizungumza na baadhi ya wachezaji wapya walijitokeza kujaribiwa Simba

King Kibadeni (wapili kulia) akiteta na Amri Said wakati walipokuwa wakizungumza na wachezaji waliojitokeza kuwania kusajiliwa Simba ambao jana walipimwa na kocha huyo.

Kocha Abdallah Kibadeni (kulia) akiwa na wasaidizi wake, Jamhuri Kihwelu 'Julio' na Seleman Matola wakiwa kwenye  mazoezi ya timu hiyo asubuhi ya leo katika uwanja wa Kinesi.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala akiteta na makocha wa timu yao, Abdallah KIbadeni (kulia) Jamhuri Kihwelu 'Julio' na Seleman Matola.

Kocha msaidizi, Seleman Matola akigawa jezi kwa wachezaji waliojitokeza kutaka kusajiliwa Simba asubuhi ya leo kwenye uwanja wa Kinesi.

Wachezaji wa kikosi cha Simba B wakijifua kabla ya kuwapima wachezaji wapya wanaowania kujiunga na Simba
KOCHA maarufu aliyewahi kuwa nyota wa Simba na Taifa Stars, Abdallah Kibadeni, ameanza rasmi kazi ya kuinoa timu hiyo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili akichukua nafasi ya Mfaransa, Patrick Liewig aliyetimuliwa.
Kibadeni maarufu kama 'King Mputa' ametua Simba ikiwa ni mara yake ya nne akitokea Kagera Sugar aliyoinoa msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja katika Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni na kuifikisha timu hiyo kwenye 'Nne Bora'
Kocha huyo alianza kazi asubuhi ya leokwenye uwanja wa Kinesi, Ubungo jijini Dar es Salaam kwa kuwajaribu wachezaji wapya waliojitokeza kuwania kusajiliwa Simba wakiwemo Wakongo wanne na mmoja kutoka Msumbiji.
Kibadeni alisema amesaini mkataba wa miaka miwili kuinoa Simba na kwamba malengo yake ni kuhakikisha Simba inafika mbali katika ligi ya nyumbani na kimataifa kama ilivyo desturi yake.
Kocha huyo aliyewahi kuifikisha Simba kwenye fainali za michuano ya CAF mwaka 1993 na kufungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan, alisema kitu cha muhimu angependa apewa muda ndani ya kikosi hicho kufanya kazi zake.
"Nimetua rasmi Simba kwa mkataba wa miaka miwili na matarajio yangu ni kuifikisha mbali, ingawa watarajie lolote kwa michuano ya Kagame kwa muda uliopo wa maandalizi, lakini kwa ligi wasiwe na shaka," alisema.
Aliongeza anachopenda kwa uongozi wake ni kumpa nafasi ya kufanya kazi bila kuingiliwa, ili hata mwisho wa  siku iwe rahisi kwao kumbana.
"Hakuna jambo ambalo silipendi kama kuingiliwa kazi, kila mtu atekeleze majukumu yake kwa maana benchi ya ufundi tuachwe tuifanye kazi na wataona nini tutakachokifanya kwani najiamini naweza," alisema Kibadeni.
Kuhusu wachezaji waliosimamishwa na uongozi wa tuhuma za utovu wa nidhamu, Kibadeni alisema hawana nafasi kwake kwa madai siku zote yeye amekuwa muumini wa suala la nidhamu kwa wachezaji.
"Kama viongozi waliwasimamisha kwa utovu wa nidhamu, kwangu pia hawana nafasi ili wasije wakaniharibia kazi, nitafanya kazi na wachezaji wote walio tayari kuitumikia Simba kwa hali na mali ili ifike mbali," alisema.
Kocha huyo anayeanza rasmi kuinoa timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame itakayofanyika nchini Sudan, aliusisitizia uongozi umpe ushirikiano katika utekelezaji wa programu zake kama walivyokuwa wakifanya kwa makocha wa kigeni.
"Nikipewa ushirikiano na kutekelezewa kila ambalo nahitaji kwa maandalizi na programu ya timu naamini Simba itatisha msimu ujao, ikizingatiwa nalijua soka la Tanzania na wasaidizi nilionao ni watu wanaojua soka," alisema.
Kwa upande wa makocha wasaidizi waliompokea Kibadeni, Jamhuri Kihwelu 'Julio', Seleman Matola na Amri Said walisema wamefurahi ujio wa mwalimu huyo aliyewahi kuwanoa enzi za uchezaji na kuamini benchi la ufundi sasa limekamilika na Simba itatisha.
"Simba ijayo itatisha, nani asiyemjue Super Coach, King Kibadeni, ebu piga picha huku King, hapa Julio aaah Simba itatakata tuombe Mungu, ila tumefurahi mno kurejeshwa kwa Kibadeni Msimbazi," alisema Julio.

No comments:

Post a Comment