STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, June 13, 2013

Musonye afichua walijua Tanzania haitashiriki Kagame 2013

http://kigalisports.com/wp-content/uploads/2012/11/Nicholas-Musonye-2-300.jpg
Katibu Mkuu wa Musonye
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye amesema kuwa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) itafanyika nchini Sudan kama ilivyopangwa lakini mwaka huu klabu za Tanzania hazitashiriki katika michuano hiyo.
Akizungumza na NIPASHE kwa simu jana, Musonye alisema kuwa walishajua mapema kwamba Tanzania haiko tayari klabu zake zishiriki katika mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Juni 18 hadi Julai 2 nchini Sudan, hivyo wataendelea na timu kutoka mataifa mengine.
"Tulijua mapema kwamba klabu za Tanzania hazitashiriki michuano hii baada ya serikali ya nchi hiyo kuingiwa na hofu ya usalama wa nchi ya Sudan ambako mashindano ya mwaka huu yanafanyika. Tutaendelea na timu ambazo ziko tayari kushiriki," alisema Musonye.
"Hata kama waziri asingesema leo (jana), tulishajua tangu mapema kuwa hawashiriki, lakini watambue kwamba michuano hii ina kanuni zake, ukizikiuka unaadhibiwa, aliongeza Katibu Mkuu huyo." Hata hivyo, Kenya ambayo ilikuwa inawakilishwa na klabu ya Tusker, nayo ilishatuma barua Cecafa kujitoa katika michuano hiyo.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, mwaka huu yamepangwa kuchezwa katika miji miwili ya Kadugli, uliopo Kordofan Kusini na Alfashery, uliopo Darfur Kaskazini, eneo ambalo kwa muda mrefu limekumbwa na vita vya wenyeji.
Juni Mosi mwaka huu akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe alisema kuwa hali ya usalama mjini Darfur ni ya wasiwasi kwa sababu watu wanaokwenda huko wanapokewa na vikosi vya magari ya jeshi na huvishwa nguo ambazo hazipenyezi risasi.
Timu tatu za Tanzania wakiwamo mabingwa watetezi wa kombe hilo, Yanga, mabingwa wa mwaka jana, Simba na Super Falcon ya Zanzibar ni miongoni mwa timu 13 zilizotakiwa kushiriki katika michuano hiyo mwaka huu.
Mapema jana, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema kuwa baada ya kuzungumza na Waziri Membe jana asubuhi Bungeni Mjini Dodoma na kuelezwa kuwa hali ya usalama Darfur ni mbaya, hayuko tayari kupeleka timu yake katika mashindano hayo.
"Nimezungumza na Waziri Membe na Naibu Waziri wa Wizara yenye dhamana na michezo (Amos Makalla) leo (jana). Waziri Membe amesema Sudan si shwari, hivyo klabu ya Simba haitapeleka timu katika michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu. Hilo ndilo tamko rasmi la Simba baada ya kuhakikishiwa na waziri," alisema Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM).
Hata hivyo, simu ya Waziri Membe ilikuwa haipatikani jana kuzungumzia suala hilo. Tanzania ina kikosi maalum kinachoshiriki kulinda amani nchini Sudan.

Chanzo:NIPASHE

No comments:

Post a Comment