STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 7, 2013

Nagy Kaboyoka kugombea tena Same Mashariki

Nagy Kaboyoka

LICHA ya kugaragazwa mara mbili na mpinzani wake ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, aliyekuwa mgombea wa ubunge wa jimbo hilo kupitia CHADEMA, Naghenjwa 'Nagy' Kaboyoka, amesema hajakata tamaa na badala yake anajipanga kuwania tena katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.
Nagy aliangushwa na Kilango katika uchaguzi wa ndani wa CCM mwaka 2005 wakati wakiwania uteuzi wa jimbo hilo kupitia CCM kabla ya mwaka 2010 kuhamia CHADEMA na kuchuana tena na kuangushwa katika uchaguzi uliodaiwa ulitawaliwa na malalamiko makubwa ya uchakachuaji wa kura.
Mwanamama huyo amesema pamoja na kufanywa mtimanyongo katika masuala ya kisiasa hajakata tamaa kwani anajipanga kushiriki uchaguzi ujao akiamini bahati itakuwa yake kutokana na ukweli anakubalika na wakazi wa jimbo hilo licha ya kushindwa kwenye uchaguzi uliopita.
Nagy alisema changamoto alizokutana nazo katika chaguzi mbili zilizopita za 2005 na 2010 imemchochea na kumpa nguvu zaidi ya kuwapigania wakazi wa jimbo hilo ambao, licha ya ahadi lukuki toka kwa chama tawala mambo bado yapo vile vile.
"Sijakata tamaa na harakati zangu za kuwatumikia wananchi, changamoto nilizokutana nazo zimezidi kunipa nguvu na kiu ya kujikita zaidi katika siasa, ili kuja kuwatumikia wananchi na hata kama sintapata bado nitaendelea kuwasaidia wananchi wenzangu kama ninavyofanya sasa kupitia asasi yangu ya WOYEGE," alisema.
Kuhusu uchaguzi uliopita, Mwanamama huyo alisema hataki kusema lolote kwani ataonekana anaendelea kulalamika, lakini wakazi wa jimbo wanajua kitu gani kilifanyika na anao,mba uzima na afya ifike 2015.
"Mimi unajua siyo mtu wa maneno, mie ni mtu wa vitendo ndiyo maana sitaki kuzungumzia kilichotokea kwenye uchaguzi uliopita kila mtu anafahamu kilichofanyika, najipanga kwa uchaguzi ujao panapo majaliwa kama chama changu kitanipendekeza tena," alisema Nagy.
Aidha aliongeza kuwa, harakati zake za kuwasaidia wananchi wa jimbo hilo kupitia asasi yake haina maana ni mipango ya uchaguzi ujao, bali amekuwa akifanya hivyo hata alipokuwa akifanya kazi Ubalozi wa Denmark akiamini ana wajibu wa kuwatumikia wananchi hata nje ya masuala ya kisiasa.

No comments:

Post a Comment