STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, August 17, 2013

Kocha Mpya JKT Ruvu hana mchecheto

Kocha Mbwana Makatta

KOCHA Mkuu mpya wa JKT Ruvu, Mbwana Makatta ameapa kurekebisha makosa yaliyoigharimu timu hiyo katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akiionya Mgambo JKT ya Tanga isitarajie mteremko wiki ijayo katika pambano lao la fungua dimba la Ligi Kuu litakalochezwa Mkwakwani jijini Tanga.
Makatta aliyetua katuika kikosi hicho kuchukua nafasi ya Charles Kilinda aliyejiuzulu katikati ya msimu uliopita baada ya JKT Ruvu kufanya vibaya na kupokewa kwa muda na kocha Kennedy Mwaisabula, alisema kitu anachoomba kwa wana JKT ni ushirikiano na nguvu ya pamoja kuweza kuiwezesha timu yao ifanye vyema.
Kocha huyo alisema mara baada ya kutua katika timu hiyo amejaribu kuweka mambo sawa kati ya yale yaliyoigharimu JKT Ruvu na kuyumba msimu uliopita na kwa muda wa maandalizi waliyofanya kwa kiasi fulani mambo yametengemaa na wapo tayari kwa 'vita'.
"Tunaamini hatuwezi kurejea makosa ya msimu uliopita, pia itambuliwe kila kocha na falsafa yake na mimi nimetua JKT nikiwa na malengo yangu na hasa kuhakikisha naifikisha mahali pazuri timu hii, ila naomba kupewa ushirikiano wa kutosha kufanikisha hayo," alisema.
Aliongeza kwa maandalizi waliyofanya wakati wa kujiandaa na ligi hiyo wanaamini kikosi chake kimewiva kuikabili Mgambo JKT katika mechi ya ufunguzi Agosti 24 na nyingine za ligi hiyo na wamepania kuhakikisha wanapata ushindi kwa kila mechi ili angalau duru la kwanza litakapoisha wawe katika nafasi nzuri.
"Tutaanzia  ugenini katika mechi yetu ya kwanza, lakini hilo halitutishi tutaenda kwa dhamira moja ya kusaka ushindi dhidi ya Mgambo JKT," alisema Makatta kipa wa zamani wa Tukuyu Stars na Yanga.
Baada ya mechi hiyo vijana hao wa JKT Ruvu watarejea nyumbani uwanja wa Mabatini-Mlandizi Pwani kuikaribisha Prisons ya Mbeya katika mchezo wake wa pili.

No comments:

Post a Comment