STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, August 21, 2013

Veterani kuchuana Tamssha la Gym, Victoria Sound kumwaga burudani

Bwendi ya Victoria Sound itakayopamba Tamasha la Home Gym
TIMU za soka za maveterani na klabu za jogging za mkoa wa Dar es Salaam zinatarajiwa kuchuana na kupamba tamasha maalum la kuadhimisha miaka 15 ya kituo cha mazoezi cha Home Gym litakalofanyika wiki ijayo jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo litakalohusisha michezo mingine kama ya kutunisha misuli, kunyanyua vitu vizito, kukimbiza wanyama kama kuku, kanga na sungura litafanyika Agosti 31 kwenye kiwanja cha Mwenge, Dar es Salaam na litapambwa na burudani toka bendi ya Victoria Sound inayotamba na nyimbo kama 'Shamba la Bibi'.
Mkurugenzi wa Home Gym, Andrew Mwangomango aliiambia MICHARAZO kuwa kituo chao kimeandaa tamasha hilo kuadhimisha mafanikio yao tangu kilipoanzishwa rasmi mwaka 1998.
Mwangomango alisema tamasha hilo litaenda sambamba na burudani na michezo mbalimbali ikishirikisha klabu za maveterani na jogging na kutaja baadhi yake kuwa ni Mwenge Shooting, Mabenzi, Survey, Meeda, Mapambano, 501 Veterani, Home Gym wenyewe, Coca Cola Veterani, NMB Veterani, Magenge 20 Jogging Team, Kingungi Jogging na nyingine.
Mwangomango alisema kwa upande wa soka mshindi atazawadiwa mbuzi beberu huku upande wa watunisha misuli na kunyanyua vitu vizito na michezo mingine pia watazawdiwa.
"Kwa sasa tunafanya mipango kwa ajili ya mgeni rasmi atakayejumuika nasi katika tamasha hilo ambalo mbali na kusherehekea miaka 15 ya kituo chetu, lakini lina lengo la kujenga umoja, urafiki na kufahamiana miongoni mwa wanamichezo wa jijini Dar es Salaam," alisema.
Aliongeza kuwa kwa upande wa burudani wanatarajiwa tamasha lao kupambwa na bendi ya Victoria Sound baada ya bendi waliyoikusudia awali ya Extra Bongo siku hiyo ya Agosti 31 kuwa na majukumu mengine.
"Tulipanga Extra Bongo ya Ally Choki ndiyo itumbuize siku hiyo, lakini ratiba hiyo inaingilia na kazi watakayoifanya siku kama hiyo kwenye viwanja vya Posta katika tamasha la mashule," alisema Mwangomango.

No comments:

Post a Comment