STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 5, 2013

Hawa ndiyo waliofungwa nje ya nchi kwa dawa za kulevya


Haya ni maelezo binafsi ya Mheshimiwa Ester Amos Bulaya bungeni Dodoma November 4 2013 kuitaka serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya dawa za kulevya na kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia wahalifu wa dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 28(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2013, napenda kutoa maelezo binafsi ya juu ya tatizo sugu la uagizaji, uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya linaloongezeka kwa kasi kubwa nchini, lengo likiwa ni kuitaka serikali ifanye mabadiliko/marekebisho ya sheria ya Dawa za kulevya na kuanzisha Mahakama Maalum kushughulikia wahalifu wanaojihusisha na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Nimeona ni wakati muafaka kutoa maelezo haya, ili Bunge lako tukufu na Serikali ipate fursa ya kuona uzito wa tatizo hili kutokana na ukweli kwamba katika miaka ya karibuni tatizo la dawa za kulevya katika nchi yetu limeongezeka kwa kasi ya ajabu hali inayopelekea athari kubwa za kiuchumi, kijamii na kiafya. Na mbaya zaidi kundi kubwa linaloathirika ni kundi la vijana, ambao ndio nguvu kazi ya Taifa letu. Na mbaya zaidi sasa hivi, wafanya biashara hawa wa dawa hizi haramu wameanza kuwatumia watoto wa shule za msingi chini ya falsafa yao mpya “wapate wakiwa wadogo…wafanye watumwa wa dawa za kulevya… na kupata uhakika wa soko la baadae pale ambapo watakuwa wameajiriwa au wamejiajiri”.
Mheshimiwa Spika,
Tafiti za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba kuna ongezeko kubwa na la kutisha katika matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin na kwa njia ya kujidunga katika nchi za Kenya, Libya, Mauritius, Shelisheli na Tanzania. Halikadhalika, Ripoti ya mpya ya hivi karibuni ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na mihadarati na uhalifu (UNODC) imetamka bayana kwamba Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa za kulevya katika nchi za Afrika Mashariki, na Mkoa wa Tanga ukitajwa kama mkoa hatari zaidi!
Mheshimiwa Spika,
Ripoti hiyo inasema jumla ya Tani 64 za dawa za kulevya aina ya Heroin ilisafirishwa bila kukamatwa kwenda au kupitia Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania kati ya 2010 na 2013. Na kwa Mkoa wa Tanga, ambao umetajwa wazi kama eneo hatari zaidi Afrika Mashariki wastani wa ukamataji wa shehena za dawa za kulevya eneo hilo umefikia KG 1,011 mwaka 2013 toka KG 145 mwaka 2010. Na kwamba Dola za Kimarekani takriban milioni 160 zinatumiwa na Watanzania na wakenya kila mwaka kwa utumiaji na usafirishaji kwa mwaka!Hili sio jambo la kufumbia macho, lazima tuchukue hatua sasa.
Mheshimiwa Spika,
Lazima tuchukue hatua sasa, kwa sababu kama nilivyoainisha hapo juu kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu tu (2010-2013), wakati Tani 64 za dawa za kulevya zilipita bila kukamatwa…zikiwa mtaani zikiharibu vijana na watoto wetu katika kipindi hicho hicho, kiasi kilichoweza kukamatwa ni tani 1.6 tu! Takwimu hizo za kutisha zinatoa picha kwamba sehemu kubwa ya shehena za dawa za kulevya hupitishwa bila kugundulika au kukamatwa na vyombo vya dola!
TASWIRA YA NCHI KATIKA JUMUIYA YA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika,
Maelfu ya watanzania wanatumikia vifungo mbali mbali ikiwamo vifungo vya maisha nje ya nchi, wengine wengi wamepoteza maisha kwa kunyongwa. Nitatoa mifano michache; China peke yake inasemekana kuna wafungwa 176 (99% – dawa za kulevya) , Brazil kuna wafungwa zaidi ya 103 na Hong Kong kuna zaidi ya watanzania 200 wenye kesi za dawa za kulevya, ambapo 130 zimeshakwisha hukumiwa na kesi 70 zikiwa zinaendelea!
Mheshimiwa Spika,
Aibu ya hivi karibuni, ambayo hatuwezi kuikwepa ni meli iliyosajiliwa Tanzania (upande wa Zanzibar- MV Gold Star ) iliyoripotiwa kukamatwa nchini Italia ikiwa imesheheni tani 30 za dawa za kulevya zenye thamani ya pauni milioni 50 ( sawa na bilioni 123 za Kitanzania). Mheshimiwa Spika, uhalifu huu, unaofanywa na mtandao huu wa watu wachache, lakini wenye nguvu umewafanya watanzania wanaokwenda nje ya nchi kudhalilika kutokana na upekuzi unaofanywa dhidi yao kwa hofu kwamba yawezekana na wao wamebeba dawa hizo haramu.
HALI YA DAWA ZA KULEVYA
Mheshimiwa Spika,
Changamoto ya dawa za kulevya sio tatizo letu peke yetu ni tatizo ambalo hata Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikipambana nalo kwa kipindi kirefu kwani tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 5 ya idadi ya watu wazima duniani (watu takribani milioni 230) wanakadiriwa kutumia dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Tukiwa sehemu ya Jumuiya hii ya Kimataifa, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kuwa tarehe 19 Desember, 1988 Jumuia ya Kimataifa ilipitisha Mkataba wa kupambana na dawa za kulevya yaani United Nations Convention Against Illicit Traffic in Narcotic Drugs and Psychotropic Substances. Tanzania ni sehemu ya Mkataba huo na hili limewekwa wazi hata kwenye kifungu cha 55 cha Sheria ya kuzuia dawa za kulevya [sura 95 ya sheria zetu kama zilivyorekebishwa mwaka 2002]. Mkataba wa mwaka 1988 ulikuwa unakazia zaidi Mkataba wa mwaka 1961 (Single Convention on Narcotic Drugs, 1961), Itifaki (Protocol) za 1972 zilizofanyia marekebisho Mkataba wa mwaka 1971 (Convention on Psychotropic Substances, 1971). Licha ya juhudi zote, tatizo la uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya, limezidi kuwa kubwa.
HALI YA DAWA ZA KULEVYA NCHINI NA MADHARA KWA AFYA YA BINADAMU
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 1995 tulitunga Sheria ya kuzuia biashara ya dawa za kulevya ambayo ilianza kufanya kazi mwaka 1996 kupitia GN.No.10/1996. Sheria hiyo inatumika Bara na Zanzibar. Kabla ya Sheria hiyo tulikuwa tuna Sheria iitwayo the Dangerous Drugs Ordinance (Cap.95). Pamoja na kutungwa kwa Sheria mpya, tatizo la dawa za kulevya limeendelea kuwa kubwa zaidi hapa nchini. Ukamataji wa dawa za kulevya kwa miaka ya nyuma ilikuwa kidogo na idadi ya walioathirika (mateja) ilikuwa ni ndogo kulinganisha na sasa hivi.
Mheshimiwa Spika,
Ni kwa bahati mbaya sana, licha ya ukubwa wa tatizo, pamoja na athari zake kwa jamii ya Watanzania, hakuna tafiti zinazoonyesha ukubwa wa tatizo kwa Nchi nzima, tafiti nyingi zilizofanywa zimejikita katika maeneo machache yaliyoathirika zaidi na dawa za kulevya . Tafiti zinaonyesha kwamba Dawa zinazotumika kwa wingi ni bangi, mirungi, heroine, mihadarati, vidonge na cocaine.Tafiti iliyofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na mapambano dhidi ya dawa za kulevya UNODC (United Nations Office on Drugs and Crime) zinaonyesha kwamba 0.2% ya Watanzania, ambao ni karibia watu milioni 1.2 wameshawahi kutumia dawa za kulevya aina ya heroine.
Mheshimiwa Spika,
Halikadhalika Shirika la afya duniani (World Health Organisation -WHO) inaripoti kuwa takribani 0.2% ya Watanzania wameathirika na Ugonjwa wa TB na takwimu za kitaifa katika program ya Kifua Kikuu na Ukoma Tanzania zinaonyesha maambukizi ya TB ni 0.4% wakati tafiti katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili inaonyesha kwamba maambukizi ya TB kwa wanaotumia dawa za kulevya ni 11% ambayo ni mara 44 zaidi ya kiwango cha maambukizi kwa watu ambao hawatumii dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa maambukizi ya UKIMWI takwimu za mwaka 2011/2012 za TACAIDS zinaonyesha kwamba 5.1% ya Watanzania wameathirika na virusi vya UKIMWI wakati tafiti ndogondogo zinaonyesha maambukizi ya virusi ya ukimwi kwa watu wanaotumia dawa za kulevya ni mara 10 zaidi ya maambukizi ya kawaida. Kwa mfano 51.9% ya wanaotumia dawa za kulevya kwa njia kujidunga sindano, 37% wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kuvuta na kufanya biashara ya ngono na 22.6% kwa wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kuvuta.
Mheshimiwa Spika,
Madhara ya kiafya kwa utumiaji wa dawa za kulevya sio tu katika magonjwa ya TB na maambukizi ya virusi vya ukimwi, bali pia katika homa ya ini. Japokuwa hakuna tafiti za kitaifa zilizofanyika kuhusiana na mchango wa matumizi ya dawa katika homa ya ini, tafiti ndogondogo za mwaka 2012 zinaonyesha kati ya 65% mpaka 75.6% ya watumiaji wa dawa za kulevya wameathirika kwa homa ya Ini, hasa homa ya ini aina ya Hepatitis. Homa ya ini ni hatari sana katika kupata magonjwa sugu ya ini ikiwepo kansa ya ini na ini kushindwa kufanya kazi.
UKUBWA WA TATIZO NA UTENDAJI WA VYOMBO VYA DOLA
Kesi kubwa ya kwanza inayohusu dawa za kulevya ni ile ya mfanyabiashara NURDIN AKASHA @HABAB V.R [1995] TLR. 227 (CAT) ambaye tarehe 20/7/1993 alikamatwa nyumbani kwake Msasani village akiwa na paketi 105 za menthaqualone (mandrax) alizo ziingiza nchini kutoka Mombasa akitumia malori yake. Sasa hivi tunaongelea uingizaji wa kilo kadhaa za dawa za kulevya na siyo paketi tena. Mwezi Machi, 2010 kilo 92 za dawa za kulevya aina ya Heroine zilikamatwa maeneo ya Kabuku Mkoani Tanga na tayari washitakiwa 5 wanatumikia kifungo. Tarehe 19/12/2010 kilo 50 za dawa za kulevya aina ya Heroini zilikamatwa tena wilayani Handeni Mkoa wa Tanga. Mwezi Septemba, 2011 kilo 179 za dawa za kulevya aina ya Heroini zilikamatwa Dar es salaam, tarehe 14/6/2011 Kilo 35 za dawa za kulevya aina ya Heroine zilikamatwa mkoani Mbeya na tarehe Januari kilo 211 za dawa za kulevya zilikamatwa mkoani Lindi.
UTENDAJI WA OFISI YA DPP
Natambua jitihada zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali ya awamu ya nne katika vyombo vya dola kwa kufanikisha jitihada za kuwakamata watuhumiwa wanaojihusisha na dawa za kulevya. Kutokana na jitihada hizo, kuanzia mwaka 2008 mpaka mwaka huu wa 2013 watuhumiwa wa dawa za kulevya ni kama ifutavyo:-
i) Cocaine kilo 395 zilikamatwa na washitakiwa waliokamatwa ni 1074
ii) Heroini kilo 768.8 na washitakiwa waliokamatwa ni 1130,
iii) Mirungi kilo 56,562 na washitakiwa waliokamatwa ni 3,712,
iv) Bangi kilo 487,472 sawa na tani 487 na washitakiwa waliokamatwa ni 20,255
v) Mandrax kilo 5 na gramu 9 na washitakiwa waliokamatwa ni 20.
Licha ya juhudi za baadhi ya watendaji waaminifu kuwakamata watu walioko katika mtandao huu hatari kumekuwa na hujuma za dhahiri dhidi ya wanaopambana na dawa za kulevya. Moja kati ya ofisi inayoshutumiwa kuwa na maafisa wanaoshirikiana na wanamtandao, ni ofisi ya DPP
MTANDAO KATIKA OFISI YA DPP NA MAHAKAMA
Natambua kazi nzuri na jitihada zinazofanywa na baadhi ya watumishi wazalendo kwa upande kwa Ofisi ya Muendesha Mashtaka, Majaji na Mahakimu waaminifu. Lakini katika ofisi hizo za umma, kumekuwa na baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakihujumu kesi za dawa za kulevya kwa kushirikiana na watuhumiwa katika kupanga jinsi ya kuwasaidia washinde kesi kwa kuwapatia taarifa za siri zinazohusiana na ushaidi na jinsi ya kuharibu ushahidi nzima.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na kupanuka kwa mtandao huu wa kuhujumu, licha ya kushirikiana na washitakiwa, mtandao uliopo katika Ofisi hiyo ya DPP umekuwa ukituhumiwa kufanya njama za kushirikiana na baadhi ya watumishi wa mahakama hasa Majaji kuhamisha kesi kupeleka kwa Majaji ambao wanadaiwa kuhusika na mtandao huu (sihitaji kutaja majina ya Majaji hapa, baadhi yao wanafamika na wengine wametajwa mara kadhaa na vyombo vya habari).
Mheshimiwa Spika,
Kwa kutumia mtandao huo, baadhi ya Majaji wamekuwa wanatafsiri sheria kwa jinsi wanavyotaka na kuwapa dhamana watuhumiwa wa kesi za dawa za kulevya ambazo hazina dhamana. Mfano mzuri ni kesi Na.6/2011, Jamhuri dhidi ya Fred William Chonde na wenzake ambao walikutwa na kilo 179 za Heroine yenye thamani ya shilingi Bilioni 6.5. Washitakiwa hawa wanashitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya ambalo kwa mujibu wa kifungu cha 148(5)(a)(ii) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai pamoja na kifungu cha 27(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya halina dhamana. Kwa tafasiri yoyote ile aliyokuwa nayo mheshimiwa Jaji, bado asingewapa dhamana kwani kifungu cha 148(5)(a)(iii) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya kinazuia dhamana kwa kosa ambalo thamani ya dawa za kulevya inazidi shilingi milioni kumi.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na Mahakama kutoa dhamana, washitakiwa wawili raia ya Pakistani wametoroka na hawapo tena nchini. Aidha, katika kesi ya R. v. Mwinyi Rashid Ismail @Mkoko, (KLR /IR 4143/2011), mshitakiwa aliomba dhamana Mahakama Kuu wakati kesi ilikuwa bado ipo Mahakama ya Kisutu ndipo wakili wa Serikali akamwambia jaji kuwa anaomba kuifuta.
Mheshimiwa Jaji huku akifahamu kuwa kesi hiyo imefika mbele yake kwa ajili ya kusikiliza maombi ya dhamana tu, na kuwa ilikuwa haijafikishwa Mahakama Kuu kwa taratibu wa sheria, aliamua kumfutia kesi mshitakiwa na kuamuru kuwa yuko huru. Sambamba na hilo, katika kesi No. 794/2011 katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Mheshimiwa Hakimu aliwafunga kifungo cha nje kwa miezi kumi na tano washikiwa Abdurahman Shaban Sindanema, said Nassoro Khamis na Abdurahim Haroub Said waliokiri kosa la kuuza na kusambaza dawa za kulevya aina ya Heroini.
Mheshimiwa Spika,
Adhabu iliyotolewa na Hakimu huyu, haipo kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya kuzuia dawa za kulevya, adhabu iliyowekwa kwa wauzaji au wasambazaji wa dawa za kulevya ni kifungo cha maisha na si chini ya miaka ishirini (20) jela kwa kipindi hicho. Kesi nyingine ni Na. 274/2005 Jamhuri dhidi ya Yusuph Hashim Nyose aliyekamatwa na kilo 1.3 za dawa za kulevya aina ya Heroine alizokuwa amemeza na kisha kuzitoa kupitia njia ya haja kubwa baada ya kukamatwa na zilikuwa na thamani ya shilingi milioni kumi na mbili na laki sita (12,600,000/=). Pamoja na ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi sita(6) wa upande wa Jamhuri ikiwa ni pamoja na mkemia aliyethibitisha kuwa ni dawa za kulevya na mashahidi walioshuhudia mshitakiwa akizitoa kwa njia ya haja kubwa, Hakimu alimuachilia huru.
Mheshimiwa Spika
Katika hukumu yake Hakimu alisema kuwa ameridhika kuwa hizo ni dawa za kulevya na zina madhara kwa binadamu na kuwa hana ubishi kuwa mshitakiwa alikutwa nazo. Hata hivyo alimuachilia huru kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuelezea mbinu walizotumia kumgundua mshitakiwa kuwa alikuwa amebeba dawa za kulevya kabla ya kumkamata. Mfano mwingine ni hukumu iliyotolewa tarehe 4/5/2007 inayoihusisha Jamhuri dhidi ya Chriswell Simon Mobini (561/2007) ambapo mtuhumiwa alikamatwa tarehe 9/4/2007 katika uwanja wa JKNA akiwa na pipi 93 aina ya heroine yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30 za kitanzania. Baada ya kufikishwa Mahakama ya Kisutu na kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu 16 (1) (b) (i) cha dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Katika shauri hili, Hakimu alimwachia huru baada ya mshtakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 1 za kitanzania kwa maelezo kwamba kwa kumtazama tu mtuhumiwa, anaonekana ni mgonjwa wa vidonda vya tumbo na hivyo hawezi kupata huduma nzuri iwapo atapelekwa rumande! Hii ni mifano michache tu kati ya mingi iliyopo!
KESI ZILIZOKO MAHAKAMANI
Mheshimiwa Spika,
Kama nilivyoainisha hapo juu, na ili kuonyesha msisitizo naomba nirejee takwimu husika kama ifuatavyo, kwamba kati ya watuhumiwa 26,191 waliokamatwa mpaka sasa kuna jumla ya kesi 89 tu zinazosubiri kusikilizwa Mahakamani. Katika vikao vya Mahakama Kuu vilivyokaa kuanzia mwezi Augosti hadi Octoba, 2013 hakuna kesi hata moja ya dawa za kulevya iliyosikilizwa na kutolewa hukumu, japo zilikuwa zimepangwa.
DHANA YA UHURU WA MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika,
Natambua kuwa Mahakama ni muhimili unaojitegemea katika kutenda shughuli zake na iko huru. Natambua pia kuwa Bunge haliwezi kuingilia shughuli za Serikali au Mahakama. Lakini pamoja na uhuru huo, Bunge hili limekuwa linakosoa Serikali pale linapoona imekosea. Kwa ujumla lazima kuwe na checks and balance. Pamoja na mapungufu niliyoelezea hapo juu kuhusiana na mwendendo wa Mahakama katika kusikiliza kesi za dawa za kulevya, Mahakama imekuwa inafanya kazi zake bila kukosolewa na chombo kingine na ndiyo maana baadhi wamekuwa wakitumia dhana ya uhuru wa Mahakama vibaya.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na matumizi mabaya ya uhuru wa Mahakama kwa baadhi ya watumishi wa Mahakama, ni mapendekezo yangu kwamba Serikali iunde tume maalumu ya kiuchunguzi kuchunguza mwenendo wa kesi hizi za dawa za kulevya ili watakao bainika kuwa wametumia nafasi /wadhifa/ madaraka yao vibaya wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka waliyonayo. Kwa kufanya hivyo, itaonyesha kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Na itakuwa ni fundisho kwa wengine. Na taarifa ya Tume iletwe katika Bunge lako tukufu kwa hatua zaidi.
KESI KUSIKILIZWA NA MAHAKIMU WASIO NA MAMLAKA
Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla watuhumiwa wote wanaokamatwa wakisafirisha dawa za kulevya hutakiwa kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu 16(1)(b)(i) cha sheria ya dawa ya kulevya. Kosa hili halina dhamana na husikilizwa na Mahakama Kuu peke yake. Hata hivyo baadhi ya Mahakimu wamekuwa wakilisikiliza kesi hizo na wengine kushirikiana na waendesha mashtaka hubadilisha hati ya mashtaka na kufanya wawe na mamlaka ya kusikiliza kesi hizo. Mfano ni shauri la Jamhuri dhidi ya Shirima (CC 433/2009).
Mheshimiwa Spika,
Katika shauri hili Mtuhumiwa alikamatwa tarehe 02/05/2009 katika Bandari ya Dar es salaam akiwa na kilo 1 ya heroine yenye thamani ya Tshs. 18,000,000/=….Tarehe 05/05/2009 alifikishwa Mahakamani na kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu cha 16(1)(b)(i) cha sheria ya dawa ya kulevya, tarehe 9/05/2009 hati ya mashtaka ilibadilishwa na mashtaka kuwa chini ya kifungu 12(d) ya sheria ya dawa za kulevya . Tarehe 14/7/2009 aliamriwa kulipa faini ya Tshs. 4, 000,000. Ubadilishwaji wa vifungu vya sheria katika hati ya mashtaka hulenga kuwasaidia watuhumiwa washtakiwe na makosa madogo badala ya yale makubwa yenye adhabu kubwa kisheria.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 16(1)(b)(i) cha sheria ya dawa za kulevya kinataja kosa la dawa za kulevya kuwa kosa ambalo halina dhamana. Hivyo waendesha mashtaka kwa kushirikiana na watuhumiwa hupendelea kuwafungulia mashtaka madogo chini ya kifungu cha 12(d) cha sheria ya dawa za kulevya. Katika kesi ambazo watuhumiwa walifunguliwa mashtaka chini ya vifungu ambavyo haviendani na makosa yao halisi , Mahakama zimekuwa zikitoa adhabu ndogo ya faini na kuwaachia huru! tena katika mazingira mengine kutoa hukumu ndogo kuliko ambayo imeainishwa katika sheria.
MAPUNGUFU YA SHERIA
Mheshimiwa Spika,
Sheria ya kuzuia dawa za kulevya haina adhabu kwa mtu anayesafirisha au anayekutwa na kemikali bashirifu (Chemical precursors). Kemikali hizi ni muhimu sana katika kutengeza dawa za kulevya aina ya Heroin na Cocaini, crystal-methamphetamine. Muathirika wa dawa crystal-methamphetamine hawezi kutibika maishani mwake (Permanent Brain Damage). Kwa sasa hivi kuna wimbi kubwa la uingizaji wa kemikali hizo zinazoenda kuangamiza nguvu kazi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa matukio ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hizo ni kesi ya Saada Ally Kilongo aliyekamatwa uwanja wa ndege wa J.K. Nyerere akiwa na 10 kilo za Ephedrine. Nyingine ni kesi ya Agnes Gerald Delwaya (Masogange) na mwenzake waliokamatwa Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za Ephedrine. Aidha, Rumishaeli Mamkuu Shoo na mwenzake wamekamatwa kwenye Kiwanda cha kutengeza Ephedrine nchini Kenya na tayari alikuwa na kilo hamsini (50) za kemikali hizo. Hawa watu licha ya madhara makubwa waliolitelea Taifa, wako mtaani wanapeta na kujipongeza!
Mheshimiwa Spika,
Kama hatutarekebisha sheria mapema iwezekanavyo, tutajikuta tunakuwa na kiwanda au viwanda vya kutengeneza dawa za kulevya hapa nchini. Hivyo, wauzaji badala ya kuagiza dawa hizo nje ya nchi, wataanza kutengeneza hapa na kuna taarifa kwamba pindi dawa za kulevya zinapokosekana wafanyabiashara huuza kemikali hizo na watumiaji wanatengeza wenyewe na kutumia.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kama hoja yangu ilivyoeleza, naomba Serikali ifanye mambo yafuatayo:-
1: Iunde Mahakama Maalumu, haraka iwezekanavyo itakayokuwa na jukumu la kushughulikia kesi za dawa za kulevya tu kama ilivyo Mahakama ya Biashara na iliyokuwa Mahakama ya Ardhi.
2: Ifanye marekebisho ya sheria ya dawa za kulevya kwa kuongeza makosa ya kusafirisha, kuuza au kukutwa na kemikali bashirifu
3: Iundwe Tume ya kuchunguza baadhi ya watendaji wa Mahakama na Serikali ambao kwa makusudi wamekuwa wakihujumu kesi za dawa za kulevya pamoja na jitihada za Serikali katika kupambana na biashara hii haramu na kuleta taarifa katika Bunge hili tukufu
4: Kiundwe haraka chombo huru chenye nguvu na mamlaka kamili kitakachokuwa na dhamana ya kupambana na dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment