STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 5, 2013

Ashanti Utd kumaliza vipi duru la kwanza kwa Simba?

Ashanti United
Simba
ASHANTI United iliyorejea Ligi Kuu Tanzania Bara ya kushuka mwaka 2007 iliianza ligi hiyo kwa aibu kwa kulala mabao 5-1 mbele ya Yanga na kesho itashuka dimbani kufungua mechi za duru la kwanza kwa kuumana na Simba.
Mashabiki wa kandanda wanapenda kujua klabu hiyo maarufu kama Wana wa Jiji watamaliza vipi kwa Simba, moja ya vigogo viwili vya soka Tanzania.
Walipoavaana na Yanga ilikuwa chini ya Hassani Banyai na kesho wakiivaa Simba ipo chini ya kocha mwingine Nico Kiondo, ambaye ameweza kuitoa timu hiyo katika unyonge iliyokuwa nao hapo awali, ingawa bado ipo katika ukanda wa hatari.
Simba wenyewe kwa sasa hawapo vyema baada ya kuporomoka toka kileleni mwa msimamo hadi nafasi ya nne ambapo hata kesho ikiifunga Ashanti haiwezi kutoka katika nafasi hiyo kwa vile timu zilizoitangulia zimevuka pointi ambazo itaweza kufikisha.
Simba kwa sasa ina pointi 21 na kama ikishinda itafikisha pointi 24, wakati Yanga, Mbeya City na Azam wenyewe wana zaidi ya pointi hizo.
Pambano hilo mojawapo kati ya manne yatakayochezwa kesho kuanza kufungia duru la kwanza litachezeshwa na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani na viingilio vyao vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. 
Waamuzi wasaidizi ni Abdallah Mkomwa na Rashid Abdallah wote kutoka Pwani wakati mezani atakuwa Hamisi Chang’walu.
Mbali na mechi hiyo, mapambano mengine ya kesho ni; JKT Ruvu Stars na Coastal Union (Uwanja wa Chamazi), Kagera Sugar na Mgambo Shooting (Uwanja wa Kaitaba, Bukoba) na Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Manungu, Morogoro).
Keshokutwa (Novemba 7 mwaka huu) raundi ya 13 kumaliza mzunguko wa kwanza itakamilika kwa mechi kati ya Yanga na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
Azam itakuwa mwenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Chamazi wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Rhino Rangers na Tanzania Prisons kutoka Mbeya.

No comments:

Post a Comment