STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, November 6, 2013

Simba yamaliza hasira zake kwa Ashanti, Tambwe, Mombeki nouma

Mombeki akitafuta njia ya kumtoka beki wa Ashanti huku, Haruna Shamte akiwa tayari kwa msaada (picha: Lenzi ya Michezo)

KAMA walivyoanza ndivyo walivyomaliza duru la kwanza, Ashanti United 'Wana wa Jiji' wameshindwa kuhimili hasira za 'mnyama' baada ya jioni hii kukubali kipigo cha aibu cha mabao 4-2 kutoka kwa Simba.
Ashanti Utd iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, ilikumbana na kipigo hicho kwenye uwanja wa Taifa ikiwa ni miezi karibu mitatu tangu walipolala kwa mabao 5-1 na Yanga katika mechi ya kufunga dimba la ligi hiyo.
Mabao mawili ya Betram Mombeki na mengine ya Ramadhani Singano 'Messi' na Amissi Tambwe yalitosha kuiangamiza Ashanti Utd ambayo kabla ya pambano hilo waliapa kutoa kisago kwa wapinzani wao hao.
Messi, ndiye aliyeanza kufungua karamu ya mabao ya Simba katika dakika ya 8 kabla ya Ashanti kusawazisha kwenye dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza kupitia kwa Hussein Sued.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kucharuka kwa kupata mabao ya harakaharaka kupitia Tambwe aliyefunga dakika ya kwanza tu ya kipindi hicho na kufikisha jumla ya mabao 10 katika orodha ya ufungaji bora.
Dakika ya nne baadaye Mombeki alifunga bao la tatu kabla ya kuongeza jingine dakika ya 15, wakati huo Ashanti ikiwa imerejesha bao jingine na la pili kwao kupitia mkongwe Said Maulid 'SMG' aliyevurumusha kombora lililomshinda kipa Abuu Hashim.

Kwa matokeo hayo Simba imefikisha jumla ya pointi 24 na kumaliza mechi zake za duru la kwanza, Ashanti ikisaliwa na pointi 10, huku pia ikijikuta ikimaliza pambano hilo bila kipa wake, Amani Simba kuwepo uwanjani kwa kulimwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba.
Kipa huyo alipewa kadi hiyo baada ya kuudaka mpira nje ya eneo lake akizuia kupigwa kanzu na nyota wa mchezo wa leo, Ramadhani Singano Messi.

No comments:

Post a Comment