STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 12, 2013

Rais Kikwete awalilia waliokufa ajali ya Burdan

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2013/06/Jakaya-Kikwete-na.jpg
Rais Jakaya Kikwete
          THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Lt(Mst) Chiku Galawa kufuatia vifo vya watu 12 na wengine 71 kujeruhiwa baada ya basi Na. T610 ATR la Kampuni ya Burudani lililokuwa likitokea Korogwe kwenda Dar es Salaam kupinduka katika Kijiji cha Taula mapema asubuhi ya tarehe 12 Desemba, 2013.

“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 12 vilivyotokea tarehe 12 Desemba, 2013 huku wengine 71 wakijeruhiwa, baada ya basi la Kampuni ya Burudani walilokuwa wakisafiria kutoka Korogwe kuelekea Dar es Salaam kupinduka katika Kijiji cha Taula”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Rais Kikwete amesema vifo vya watu hao ni pigo kubwa siyo tu kwa familia za watu waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo, bali pia Taifa letu kwa ujumla ambalo limepoteza nguvu kazi muhimu iliyokuwa bado inahitajika kwa ujenzi wa Taifa.

“Kutokana na msiba huo mkubwa uliotokea katika eneo la Mkoa wako, ninakutumia Salamu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu wewe Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Lt. (Mst) Chiku Galawa kwa kupoteza watu wengi kwa mara moja katika ajali hiyo.  Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu wote, Amina”.

Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Tanga kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa familia, ndugu na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao katika ajali hiyo, lakini amewahakikishia kwamba yuko pamoja nao katika kipindi hiki cha maombolezo.  Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia wakiomboleza vifo vya ndugu zao.

Aidha Rais Kikwete amesema anawaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wa ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida, ili waungane tena na ndugu na jamaa zao na kuendelea na maisha yao kama ilivyokuwa kabla ya kutokea kwa ajali.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
12 Desemba, 2013

No comments:

Post a Comment