STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 10, 2014

Full Maganga alitoa bao lake la Simba kwa mwanae

Full Maganga
MFUNGAJI wa bao pekee lililoiua Simba kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Full Maganga wa Mgambo JKT amesema bao hilo ni zawadi maalum kwa mwanae kipenzi, Jamilat (5).
Aidha amesema amejisikia faraja kubwa kuwatungua Simba kutokana na ukweli kwa muda mrefu alikuwa na ndoto za kuzifunga timu kubwa nchini na kuahidi bado zamu ya Yanga watakapoumana nao.
Akizungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu mapema leo kutoka jijini Tanga, Maganga alisema bao alilofunga juzi wakati wakiizamisha Simba kwa bao 1-0 analitoa kwa mwanae huyo anayempenda kupita maelezo.
"Bao langu la jana ni zawadi maalum kwa mwanangu kipenzi, Jamilat mwenye miaka mitano, nilijiwekea ahadi kuwa ni lazima niwatungue Simba na Mungu amenisaidia nimefurahi sana," alisema.
Aliongeza kuwa, amekuwa na ndoto za muda mrefu kuwazifunga timu kubwa na bahati imekuwa kwake na kuahidi atafanya hivyo siku timu yao itakakapoumana na Yanga.
"Bado zamu ya Yanga, naamini Mungu atanijalia kutimiza hilo kama nilivyotimiza kwa Simba na furaha zaidi ni kwamba timu yangu imepata pointi tatu muhimu tulizokuwa tunazihitaji," alisema Maganga.
Mgambo ambayo pamoja na ushindi huo bado imesalia mkiani, iliiduwaza Simba kwa kuwalaza bao hilo lililofungwa na Maganga katika dakika 28 za kipindi cha kwanza.
Pamoja na Maganga kufunga bao hilo lililomnyima raha kocha wa Simba, Zdrakov Lugarusic, lakini kazi kubwa iliyofanywa na kipa wao Salehe Tendega aliyeokoa michomo hatari ya nyota wa Simba.
Mgambo JKT itasafiri hadi mjini Tabora kuvaana na Rhino Rangers mechi itakayochezwa Jumamosi ijayo.

No comments:

Post a Comment