STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 10, 2014

TFF yawafungia wachezaji watano JKT Kanembwa


KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia mechi tatu wachezaji watano kati ya tisa wa timu ya Kanembwa JKT waliolalamikiwa na Sekretarieti kwa kumpiga mwamuzi kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyochezwa Novemba 2 mwaka jana.
Wachezaji hao ni Bariki Abdul, Mrisho Musa, Nkuba Clement, Nteze Raymond na Philo Ndonde. Wachezaji ambao hawakutiwa hatiani kutokana na ushahidi dhidi yao kutojitosheleza ni Abdallah Mgonja, Mbeke Mbeke, Ntilakigwa Hussein na Uhuru Mwambungu.
Mechi hiyo dhidi ya Stand United iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ilivunjwa na refa Peter Mujaya dakika ya 87 kutokana na kupigwa na wachezaji hao baada ya kuamuru ipigwe penalti dhidi ya timu yao.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 49 (1)(b) ya Kanuni za Nidhamu za TFF baada ya kupitia vielelezo vilivyowasilishwa na Sekretarieti ya TFF ambavyo ni ripoti ya refa, ripoti ya kamishna wa mechi hiyo na video iliyoonesha tukio hilo.
Pia kabla ya kutoa adhabu baada ya kusikiliza utetezi kutoka kwa walalamikiwa ambao ni wachezaji hao na timu yenyewe ya Kanembwa JKT. Nayo Kanembwa JKT imetiwa hatiani na kupigwa faini ya sh. milioni ambayo inatakiwa kuilipa kabla ya kucheza mechi inayofuata.
Kamati hiyo iliyokutana jana (Februari 9 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas, kwanza imelaani kitendo cha wachezaji wa timu hiyo kumzonga refa, kwani vitendo vya aina hiyo ndiyo vichocheo vya vurugu viwanjani.
Lakini pia imempongeza nahodha wa Kanembwa JKT, Mbeke Mbeke kwa kuwa mstari wa mbele kuwazuia wachezaji wenzake waliokuwa wakimpiga refa wa mchezo huo.
Vilevile Kamati hiyo imesema aliyesababisha matatizo hayo ni refa Mujaya, na ingawa ilikuwa na uwezo wa kumchukulia hatua lakini haikufanya hivyo kwa vile hakukuwa na mlalamikaji na tayari Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilishamwadhibu.
Wakati huo huo: Vyama vya Mpira wa Miguu vya mikoa vimetakiwa kuwasilisha majina ya mabingwa wao kufikia Machi 30 mwaka huu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Timu zote zitakazofuzu kucheza RCL zinaruhusiwa kusajili wachezaji wapya wasiozidi watano kutoka ndani ya mkoa kwa kufanya taratibu za uhamisho. Kamati imesisitiza kuwa usajili wa RCL ni uleule uliotumika kwenye Ligi ya Mkoa.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Februari 6 mwaka huu imekataa ombi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) kuongeza timu za Ligi ya Mkoa kutoka 20 hadi 24.
Ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange, Kamati hiyo imesema kwa mujibu wa Kanuni ya Ligi ya Mkoa, ligi hiyo inatakiwa kuwa na timu kati ya 16 na 20, hivyo vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vinatakiwa kuendesha ligi kwa kufuata kanuni.
Kamati hiyo imeongeza kuwa hata kama ingekubalia ombi la MZFA kiutaratibu lisingewezekana kwa vile kanuni hufanyiwa marekebisho baada ya msimu kumalizika, wakati ombi hilo limewasilishwa katikati ya msimu.

No comments:

Post a Comment