STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 6, 2014

Uchaguzi Mkuu Simba Waiva, Hanspope ndiyo basi tena!

Zakaria Hanspope
MSAJILI wa Klabu na Vyama vya Michezo Nchini jana aliipitisha katiba ya klabu ya Simba lakini ikiwa imeondolewa kipengele cha 26 (4) kilichokuwa kimefanyiwa marekebisho na wanachama wa klabu hiyo ambao walifanya mkutano mkuu wao Machi 16 mwaka huu kwenye ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kugonga mwamba kwa kipengele hicho kunamaanisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba wa kuteuliwa, Zacharia Hanspoppe, hataweza kuwania uongozi ndani ya klabu hiyo.
Kipengele hicho kinachoelezea sifa ya mgombea kwamba ni lazima asiwe mtu aliyewahi kufungwa/ kutiwa hatiani kwa kosa la jinai, ndiyo kilimuondoa Hanspoppe aliyekuwa anawania uenyekiti katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2010 ambao ulimuweka madarakani Mwenyekiti, Ismail Aden Rage na wenzake.
Akizungumza jana jijini, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kwamba kipengele hicho hakikufika kwa msajili na kiliondolewa na Kamati ya Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sababu inapingana na katiba ya shirikisho hilo linalosimamia mchezo huo nchini.
Kamwaga alisema kuwa kukamilika kwa katiba hiyo ni fursa kwa klabu yao kutangaza tarehe mpya ya kufanya uchaguzi utakaowaweka madarakani viongozi wapya.
Kamwaga alisema kuwa marekebisho mengine ambayo yalifanyiwa marekebisho na wanachama wa Simba yamepitishwa mojawapo ni kiongozi wa juu sasa atajulikana kwa jina la Rais badala ya Mwenyekiti na kutakuwa na Makamu wa Rais.
Alisema kuwa mabadiliko yaliyopitishwa ni pamoja na kuundwa kwa Kamati ya Rufaa, Kamati ya Maadili na pia ndani ya kata moja sasa inaruhusiwa kuwa na tawi zaidi ya moja lakini liwe na wanachama kuanzia 50 na wasiozidi 250.
Pia Kamwaga alisema kwamba kati ya wajumbe watano wa watakaochaguliwa, nafasi moja itakuwa ni kwa mjumbe mwanamke na hiyo wamelenga kuleta mawazo ya jinsi hiyo ndani ya uongozi.
"Kuundwa kwa kamati hizi kunaashiria kwamba matatizo yetu ndani ya Simba yanaweza kumalizwa na kamati hizi kabla ya kuvuka ngazi nyingine," alisema Kamwaga.
Alieleza kwamba kufuatia katiba hiyo kusajiliwa, Kamati ya Uchaguzi ambayo iko chini ya Mwenyekiti wake, Damas Ndumbaro, inatarajia kukutana leo jioni kwa ajili ya kupanga tarehe ya uchaguzi na mchakato mzima utakaohusisha zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment