STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 9, 2014

Swebe Santana kuandaa kongamano la waigizaji

MUINGIZAJI nyota nchini ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa kundi la Kaole Kwanza, Adam Malele 'Swebe Santana' amesema wapo kwenye mipango ya kuandaa kongamano kubwa la wadau wa filamu na maigizo nchini ili kujadili mambo yatakayowakomboa wasanii na wadau wa fani hizo.
Akizungumza na MICHARAZO kwenye viwanja vya Leaders wakati wa kuaga mwili wa mtayarishaji na muongozaji wa vipindi vya runinga, marehemu George Tyson, Swebe alisema kongamano litakalochukua muda wa siku mbili litafanyika jijini Dar es Salaam na litahudhuriwa pia na viongozi wa serikali wanaohusika na masuala ya utamaduni na sanaa.
Swebe alisema, lengo la kongamano hilo kusaidia kujadili na kuweka mambo sawa juu ya tasnia ya sanaa, ambayo imekuwa haina tija kwa wasanii na wadau wake kulinganisha na wale wanaozisimamia.
Alisema itakuwa nafasi nzuri ya wadau wa sanaa kuwasilisha kilio chao kwa serikali kuhusu hali ya mambo inayowakwaza na kuwaacha kinyonge sambamba na kuweka mikakati na misingi itakayowasaidia vijana wanaoibukia kwenye sanaa kwa ujumla nchini.
"Leo kila mtoto na kijana anatamani au kuota kuja kuwa msanii, lakini hali ilivyo ndani ya tasnia hiyo inahitaji kujengewa misingi ambayo itawafanya wanufaike na jasho lao kama ilivyo kwa wanasoka au wanataaluma wengine, fani yetu imepuuzwa na imekuwa kama ng'ombe ambaye anakamuliwa, bila mkamuaji kujua ng'ombe huyo amekula nini," alisema.
Swebe alisema kwa sasa wanaendelea kusaka wafadhili na wadhamini wa kuwapiga tafu kulifanikisha kongamano hilo ambalo litawahusisha pia wadau wa sanaa kutoka mikoa mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment