STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, June 22, 2014

Tanzia: Onesmo Waziri 'Ticotico' hatunaye, afa ajalini mjini Mafinga

Onesmo Waziri 'Ticotico akihiojiwa
Ticotico (kushoto) akiwa na wachezaji wenzake wa Golden Bush Veterani
Ticotico akimiliki mpira enzi za uhai wake
Jamaa alipenda soka nyie acheni
TAARIFA zilizotufikia muda huu zinasema kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa timu ya Golden Bush na mwanachama maarufu wa Simba Onesmo Waziri 'Ticotico' amefariki kwa ajali ya gari mjini Mafinga wakati akielekea kwenye michezo ya kirafiki uliokuwa uchezwe Makambako.
Mmoja wa viongozi wa Golden Bush, Geofrey Chambua alilidokeza gazeti hili kuwa marehemu alikumbana na mauti baada ya gari walilokuwa wakisafiria mjini humo kukumbwa na ajali na Ticotico kupoteza uhai wake.
Chambuia hata hivyo hakufafanua kama kuna wachezaji wengine waliokuwa kwenye msafara wao wapo katika hali gani iwapo nao walikuwa kwenye gari alilokuwa marehemu Ticotico.
Ila alisema kuwa mwili wa marehemu, aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya SMEC inayohusika na Ujenzi wa Mradi wa Magari ya Mwendo Kasi jijini Dar umehifadhiwa katika Hospitali ya Mafinga kwa ajili ya taratibu za mazishi yake.
Enzi za uhai wake Ticotico aliwahi kuwa Katibu wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya klabu ya Simba chini ya uongozi wa Ismail Aden Rage.
Ticotico aliyekuwa shabiki mkubwa wa klabu za Arsenal na Barcelona alikuwa akimiliki klabu ya Golden Bush inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu wilaya ya Kinondoni na ile ya maveterani.

Kabla ya kuamua kuanzisha klabu yake, Ticotico alikuwa akijitolea kwa hali na mali katika kufanikisha baadhi ya usajili wa wachezaji wa Simba, ikiwamo ya George Owino aliyewahi kuichezea pia Yanga na uongozi wa Rage ulipoingia madarakani mwaka 2010 ulimteua kuwa Katibu wa Kamati ya Fedha kabla ya kujiuzulu kutokana na kutingwa na majukumu binafsi.
Taarifa zaidi zitawajia, ila kwa hakika ni msiba unaumiza kwa wadau wa soka na hasa wale wa Golden Bush Veterani, Simba pamoja na rafiki zake wote akiwamo mmiliki wa blogu hii.
Kwa hakika Ticotico atakumbukwa kwa ucheshi wake na mapenzi yake katika soka na moyo wa kujitolea na ukarimu mkubwa ulioanikizwa na mwingi wa utani.
MICHARAZO Inawapa pole familia, ndugu, jamaa na rafiki pamoja na wadau wote wa soka kutokana na msiba huu. Mungu awape subira kwa kutambua kuwa kila Nafsi Itaonja Mauti na kwamba sisi sote ni wa Mola na Kwake Tutarejea Hakika. Innalillah Waina Illah Rajiun

Huu ni ujumbe wake wake wa mwisho kuhusiana na ziara yao hiyo ya michezo mjini Makambako;

Kwa niaba ya uongozi wa Golden bush veterans ambao ni mabingwa wa Tanzania Bara na visiswani yaani Mabingwa wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, napenda kuwapa taarifa kwamba timu kamili ikijumuisha kikosi cha kwanza kama kinavyoonekana katika picha hapo chini, itaondoka siku ya jumamosi alfajiri kuelekea Makambako kwa ajili ya mechi mbili yaani Makambako Veterans VS Golden Bush na Mafinga Veterans vs Golden Bush. Games zote zitapigwa uwanja Makambako Veterans siku ya tarehe 22/06/2014. Kwakutambua umuhimu na ugumu wa game hizo, Golden Bush ametanguliza watu wafuatao kwenda kuweka mambo sawa, Godfrey Chambua a k a Hans Poppe (mwanasheria na mwenyekiti kamati ya ufundi na mambo ya kale), Awilly Mshanga mchezaji mwandamizi kutoka Mbeya na Nico Nyagawa  ambaye ndiye Nahodha msaidizi wa timu yetu.


Aidha masafara wa wachezaji 28 ni viongozi watu utaondoka siku ya jumamosi. Mkuu wetu wa msafara bwana Waziri Mahadhi “Mandieta” ambaye ndie Mhazini wetu amekamilisha mambo yote ya kiutawala tayari kabisa kwasafari.


Kwa siku chache zilizobaki tutaweka camp ya muda na kufanya mazoezi ufukweni mwa bahari tayari kabisa kutoa kipigo kwa timu hizo mbili.


Tunasikitika wapenzi wetu wa Dar es salaam kwamba weekend hii hatutakuwepo kuwapa burudani hadi weekend inayofuata. Nawatakieni maandalizi mema ya mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhan.


Asanteni kwa kunisikiliza.


Onesmo Waziri

Msamaji wa timu.

No comments:

Post a Comment