Na Kipimo Abdallah
CHAMA cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania) kimekanusha tuhuma zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa ni chama kilichokuja kubomoa vyama vya upinzani hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Mawasiliano na Uenezi wa ACT -Tanzania Mohammed Massaga wakati akizungumza na mwandishi wa MICHARAZO ofisi kwake jijini Dar es Salaam.
Massaga aliomba vyama hivyo kuacha kufanya siasa nyepesi na kujikita katika hoja ili kuhakikisha kuwa upinzani unakuwa na nguvu ili viweze kukitoa chama tawala CCM madarakani.
Alitoa wito kwa watanzania kuviunga mkono vyama vya siasa ambavyo vinaonyesha ni madhubuti ya kukabiliana na ubadhirifu wa rasilimali za Taifa ili kufikia malengo ya maisha bora ambayo kwa sasa yamekwama.
Katibu huyo wa Mawasiliano na Uenezi alisema iwapo vyama vya upinzani vitakuwa na umoja na ushirikiano wa dhati zipo dadli tosha za kukiondoa chama tawala madarakani.
Alisema wapo baadhi ya viongozi ambao wanashindwa kufanya siasa na kubakia kulalamika jambo ambalo linachelewesha mabadiliko.
"Ndhani unaona mwenyewe tatizo la siasa za Tanzania ni wanasiasa kushutumiwa na kuacha kufanya siasa za kweli ambazo zinaweza kuleta mabadiliko kwa jamii ya Kitanzania" alisema
Massaga alitolea mfano wa mchakato wa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali.
Kwa upande mwingine Massaga alisema katika kujenga chama chao cha ACT- Tanzania wamefanikiwa kuvuna wachama wapya zaidi ya 11,800 katika mikoa 12 ya Tanzania Bara kwa kipindi cha mwezi Agosti mwaka huu.
Katibu huyo wa Mawasiliano na Uenezi ACT alisema kwa sasa chama hicho kina wanachama zaidi ya 187,000 nchini kote hivyo juhudi zao ni kuongeza wanachama wengi zaidi kwa kutumia itikadi yao ya demokrasia ya jamii.
Alisema chama hicho kilifanya ziara katika mikoa 12 ambayo Tanga, Singida, Shinyanga, Simiyu, Geita, Tabora, Mara, Mwanza, Lindi, Kigoma, Pwani na Mtwara ambapo wamepokelewa kwa nguvu kubwa.
Massaga alisema pamoja na kuvuna idadi hiyo ya wanachama wamefanikiwa kusimika viongozi wa muda katika majimbo 68 ya Tanzania bara na viongozi wa kata na matawi kwenye majimbo hayo.
"Kwa kifupi tumepata mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha miezi minne tangu kupewa usajili wa muda kwani kila tunapopita tunapokelewa kwa nguvu zote jambo ambalo linatupa matumaini ya kufanya vizuri kwenye chaguzi zijazo", alisema.
Katibu huyo wa Mawasiliano na Unezi wa ACT-Tanzania alisema katika kuhakikisha kuwa wanafikia malengo katika medani za siasa Tanzania wataendelea kuwaelimisha wanachama juu ya kujitokeza kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
No comments:
Post a Comment