STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, September 28, 2014

Kingunge awashushua wanaoiota Tanganyika


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg1ZYzBGLwXu0x9UUT0731EMnVXnS3ORTl2ardjjCveW-DptFDEfVH4KiZtdRSjy-RZaWJ6k-0A3U6UVSj9aE2xoIG-Si79w_J4GMZifJDM8J2GG4KTLYy16Jly2XJvEc7vHbKbLanG6w59/s1600/DSCF0347.JPG 
Na Kipimo AbdallahWAKATI suala la Utanganyika na Utanzania liendelea kukuna vichwa vya wanasiasa na wananchi wa kada mbalimbali Mwanasiasa Mkongwe Mzee Kingunge Ngombale Mwiru amewataka watanzania wasahau hilo na kujitambua kuwa wao ni Watanzania.
Kauli hiyo ya Ngombale Mwiru inakuja ikiwa ni muda mchache baada ya Mjumbe mwenzake ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la  Maalumu la Katiba John Cheyo kusema itakuwa ngumu kwa jamii kuondolewa dhana ya kuwaTanganyika haipo.
Mzee Ngombale Mwiru alisema ni jambo la kusikitisha kuona watu wanaitaja Tanganyika wakati wakijua kuwa hiyo ni historia ya aibu kwa Watanzania ambao walikuwepo katika kipindi hicho cha ukombozi wa Taifa hili.
Ngombale Mwiru alisema jambo la kushangaza wapo watu ambao hata Tanganyika hawajaishuhudia lakini wameonekana kuwa na nguvu ya kuhitaji uwepo wake jambo ambalo linapotosha jamii.
“Kwa kweli sikuwa na dhamira ya kulizungumzia suala hili ila nimeshawishika baada ya kuona mzee mwenzangu kuongea na kuonyesha kuhitaji Tanganyika jambo ambalo mimi nalipinga kwa nguvu zote kwa sababu najua historia yake haina maana kwa Watanzania wa leo” alisema.
Aidha Mzee Ngombale Mwiru alitoa wito kwa jamii kusoma historia ya nchi hii ili kuhakikisha kuwa wanapata takwimu sahihi za nchi yao ili kuacha tabia ya kufuata mkumbo ambao hauna tija kwa maslahi ya Taifa.
Akichangia katika Bunge hilo Mbunge wa Bariadi Mashariki John Cheyo alisema itakuwa ngumu kuisahau Tanganyika kutokana na ukweli kuwa ndiyo msingi wa uwepo wa Tanzania.
Cheyo alisema haiwezekani Zanzibar ikaendelea kuwepo na kutambulika na Tanganyika ikasahaulika katika mazingira ya kawaida kama baadhi ya viongozi wengine wanavyotaka.
Mjumbe huyo wa Bunge la Katiba alisema ni vema jamii ikapatiwa elimu ya kutosha ili kuhakikisha kuwa ufahamu unakuwepo wa kutosha ili kila Mtanzania aweze kuwa na uelewa juu ya nchi yao.
 Kwa upande mwingine Cheyo amewataka wabunge kutoka Zanzibar wasije kuzuia haki za Watanzania Bara wanaozidi milioni 47 wakati wa upigaji kura ili kuhakikisha kuwa Katiba hiyo inayopendekezwa inapita.
Cheyo alisema idadi ya wazanzibari ni ndogo ila ina nguvu katika mchakato mzima wa kupatikana kwa katiba ambayo itaweza kulinda muungano wa nchi au kuuvunja.
Alisema lipo suala la aina ya muungano ambalo limeweza kuleta malumbano makubwa sana katika Bunge hilo hivyo ni vema suala hilo likatafakariwa vizuri ili kuhakikisha kuwa kila upande unaridhika kwa maslahi ya Taifa.
Cheyo alisema itakuwa vizuri iwapo fursa itapatikana kwa wahusika kutoa nafasi kwa wananchi kupiga kura dhidi ya aina gani ya muungano wanaoutaka ili kuhakikisha kuwa suala hilo limetatuliwa.
Mbunge huyo wa Bunge la Katiba alitoa rai kwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati ambao wanaendelea na harakati za kuhamasisha jamii kupinga Bunge hilo waachane na mpango huo kwani wao wapo kihalali.
Alisema Kituo Cha Demokrasia (TCD) kipo hivyo wanapaswa kukitumia ili kuhakikisha kuwa wanafikia muafaka kwa maslahi ya Taifa na sio kung’amg’ania maandamano ambayo yanahatarisha maisha ya watanzania.

No comments:

Post a Comment