TIMU ya taifa ya Algeria imeweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza kufuzu katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco baada ya kupata ushindi murua wa mabao 3-0 dhidi ya Malawi katika mechi za kundi D.
Vijana wa kocha Christian Gourcuff wameweka rekodi ya kushinda mechi
zake zote mpaka sasa kukiwa kumesaliwa mechi mbili kabla ya mechi za
makundi kumalizika.
Mabao ya washindi hao waliong'olewa kwenye raundi ya pili ya Fainali za Kombe la Dunia za 2014 na waliokuja kuwa Mabingwa wapya, Ujerumani yaliwekwa kimiani naYasine Brahimi dakika ya pili, Riyad Mahrez dk ya 45 na Islam Slimani Dk ya 55.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo kundi B lilishuhudiwa Ethiopia ikiwa ugenini mjini Bamako iliicharaza wenyeji Mali kwa mabao 3-2 na kujiweka pazuri kabla ya mechi mbili za mwisho dhidi ya Algeria na Malawi.
Bakary Sako alianza kufungua milango ya pambano hilo kwa kuwafungia wenyeji bao la kuongoza dakika ya 31 kabla ya wageni kurejesha na kuongeza la pili kupitia kwa wachezaji wao Oumed Oukri na Getaneh Kebede na Mali kuchomoa na kufanya matokeo kuwa 2-2 kwa bao la Mustapha Yatabare dakika dakika ya 69.
Bao la ushindi la Ethiopia lilifungwa na Abebaw Butako Bune, huku Angola ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Lesotho katika mechi ya Kundi C.
Bastos alianza kuwaandikia wenyeji bao dakika ya pili kabla ya Ary Papel kuongeza la pili dakika ya 33 na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 2-0 na kwenye kipindi cha pili Tsoanelo Koetle alijifunga katika dakika ya 47 na Love akapigilia msumari wa mwisho kw akuifungia Palancas Negras bao dakika ya 57.
nazo timu za Burkina Faso na Gabon zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 Jonathan Pitroipa akiifungia Burkinabe na wageni kuchomoa kupitia kwa Malick Evouna dakika ya 76.
Cape Verde waliendelea kuweka ugumu katika Kundi F baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Msumbiji kwa bao la Heldon katika dakika ya 75 na kuifanya wenyeji kufikisha pointi 9, huku Msumbiji wakisalia kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 5 sawa na Zambia walioshinda nyumbani mabao 3-0 dhidi ya Niger.
Nayo timu ya Tunisia ilifuata nyayo za majirani zao Misri walioishinda Botswana kwa mabao 2-0 nyumbani baada ya kuilaza Senegal bao 1-0 bao lilifungwa 'jioni' na Ferjani Sassi na kuifanya Tunisia kuongoza msimamo wa kundi hilo wakiwa na pointi 10 wakifuatiwa na Senegal wanaokamata nafasi ya pili wamiwa na pointi saba wakiitangulia Misri wenye pointi 6 wakiwa nafasi ya tatu.
No comments:
Post a Comment