STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, October 9, 2013

Ndanda, Green Warriors hapatoshi leo FDL

Na Boniface Wambura
GREEN Warriors ya Dar es Salaam na Ndanda ya Mtwara zinaumana kesho (Oktoba 9 mwaka huu) katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo mshindi atakamata uongozi wa kundi A.

Mechi hiyo ya raundi ya tano itachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ambapo timu itakayoshinda itafikisha pointi kumi na kuipiku African Lyon inayoongoza sasa kundi hilo ikiwa na pointi tisa.

Kwa upande wa kundi B kutakuwa na mechi tatu ambapo Polisi Morogoro inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi tisa itakuwa ugenini dhidi ya Majimaji inayokamata mkia ikiwa na pointi moja. Mechi itachezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Kurugenzi itakuwa kwenye uwanja wake wa Wambi ulioko Mafinga mkoani Iringa kuikabili Burkina Faso ya Morogoro wakati Uwanja wa CCM Vwawa, Mbozi mkoani Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Kimondo na Mkamba Rangers.

Tuesday, October 8, 2013

Cheka kwenda kuhamasisha ngumi Muheza


BINGWA wa Dunia wa mchezo wa ngumibza kulipwa anayetambuliwa na WBF, Francis Cheka 'SMG' anatarajiwa kwenda kuhamasisha mchezo huo wilayani Muheza, Tanga kwa mwaliko wa kocha maarufu Charles Mhilu 'Spinks'.
Spinks aliiambia MICHARAZO kuwa Cheka ataenda kuhamamisha mchezo huo siku ya Eid El Hajj itakayoadhimishwa wiki ijayo wakati wa michezo kadhaa ya ngumi itakayofanyika kwenye viwanja vya Jitegemee, mjini humo.
Kocha huyo ambaye amekuwa akimnoa Cheka kwa nyakati tofauti alisema lengo la kumualika Cheka ni kutaka kuwahamasisha vijana wa wilaya hiyo na mkoa mzima wa Tanga katika mchezo huo.
"Sifa alizonazo katika mchezo huo ikizingatiwa ni hivi karibuni ametoka kumpiga Mmarekani na kunyakua ubingwa wa Dunia itasaidia kuwatia hamasa vijana wenye vipaji vya ngumi kujibidiisha kuwa kama yeye," alisema.
Spinks, alitoa wito kwa wadau wa ngumi kujitokeza kusaidia mchezo huo kwa lengo la kuufanya uwe na tija na kuwasaidia vijana wanaoucheza kuutumia kama ajira yao sambamba na kuliletea sifa taifa kama ilivyo kwa Cheka na wenzake.
Cheka hakuweza kupatikana kuthibitisha juu ya mualiko huo, kwa vile siku yake kutopatikana hewani pengine alikuwa darasani baada ya hivi karibuni kuanza masomo katika Shule ya St Joseph ya mjini Morogoro.