STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, October 20, 2014

Ghana, Afrika Kusini 'zaichomolea' CAF AFCON 2015

 
NCHI za Ghana na Afrika Kusini zimeichomolea kiaina Shirikisho la Soka Barani Afrika, CAF juu ya kubeba jukumu la kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika, AFCON 2015 baada ya Morocco kukwepa uenyeji kisa ugonjwa wa Ebola.
Wakati Waziri wa wa michezo wa Afrika Kusini, Fikile Mbalula amesema leo kuwa nchi hiyo haiku tayari kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika Januari mwakani kama Morocco watajivua uenyeji kwasababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, Ghana wenyewe wameweka bayana kuwa haikupanga kubeba jukumu hilo.
Inaelezwa kuwa CAF ilizifuata Afrika Kusini, Ghana na nchi zingine tano kuelekea katika mkutano wao wa Novemba 2 kuamua mustakabali wa michuano hiyo. Lakini Waziri huyo wa Afrika Kusini aliviambia vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa hawako tayari kuwa wenyeji wa michuano hiyo kwani wana majukumu ya kuhakikisha wanasaidia kupambana na kuutokomeza ugonjwa huo ambao mpaka sasa umeshaua zaidi ya watu 4,500. 
Mbalula amesema hata wakati kabla suala hilo halijapelekwa katika bunge la nchi hiyo kujadiliwa jibu lilikuwa ni hapana kwani walikuwa hawana uwezo wa kutosha kwa sasa kuandaa michuano hiyo. 
Afrika Kusini imeweza kuandaa michuano hiyo mara mbili kwa dharura, baada ya kuchukua nafasi ya Kenya mwaka 1996 walioshindwa kwa kukosa fedha na Libya mwaka jana kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Naye Rais wa Ghana, John Mahama amesema nchi bado haijafanya maamuzi kama wakubalia kuwa wenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani au la. 
Waziri wa michezo wa Ghana Mahama Ayariga ameeleza kuwa nchi hiyo ambayo imewahi kunyakuwa taji la michuano hiyo mara nne ina miundo mbinu ya kutosha kuwa mwenyeji huku kukiwa kumebakiwa miezi mitatu na wanafikiria ombi hilo la CAF. 
Kauli yake hiyo imekosolewa vikali na Chama cha Madaktari wa nchi hiyo na asasi zingine za kiraia ambao wamedai kuwa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo kunaifanya nchi nzima kuwa katika hatari ya kulipukiwa na ugonjwa huo ambao tayari umeshaua watu 4,500 mpaka sasa. 
Katika mkutano wake Mahama alipoza hofu za wananchi wa Ghana na kudai kuwa hakuna uamuzi wowote uliofikiwa mpaka sasa kuhusu kuandaa michuano hiyo inayoshirikisha nchi 16.

No comments:

Post a Comment