STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, November 15, 2013

Japhet Kaseba azidunda Australia

 
BINGWA wa Taifa wa Ngumi za Kulipwa, Japhet Kaseba 'Champion' yupo nchini Australia kwa ajili ya kupigana na bondia Jeremy van Dieman wa nchini humo katika pambano la kimataifa.
Pambano hilo la uzito wa Heavy Light  (kilo 79) linatarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Metro City, uliopo mjini Northbridge nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotumwa nchini na Kaseba akiwa Australia, mabondia hao walipimwa uzito jana tayari kwa pambano hilo la leo ambalo litakuwa la kwanza kwake kimataifa tangu aliporejee kwenye ngumi.
"Nipo Australia na tumetoka kupima uzito kwa ajili ya pambano letu la kesho (leo) la kimataifa dhidi ya mwenyeji wangu Jeremy van Dieman ambaye nitapigana naye kwenye Ukumbi wa Metro City, Magharibi mwa Australia," alisema Kaseba.
Kaseba alisema mara baada ya pambano hilo ambalo ametamba kufanya vizuri ili kujitengenezea mazingira ya kuwania ubingwa wa dunia, atarejea nchini siku ya Jumapili majira ya saa nane mchana.
"Nitarejea nchini Jumapili ya Novemba 17 saa nane mchana, nawaomba Watanzania waniombee kila la heri niweze kufanya vema katika mchezo huo wa Ijumaa (leo)," alisema Kaseba, bingwa wa zamani wa Dunia wa Kick Boxing.
Kaseba mwenye rekodi ya kucheza michezo minne akishinda miwili na kupoteza miwili, atavaana na Dieman anayeshikilia nafasi ya tisa nchini mwake kwenye uzito huo wa Heavy Light huku akicheza michezo minne na kutoka sare miwili.

Haya ndiyo majembe 32 ya Taifa Stars yatakayoivaa Harambee Stars

Kocha Kim Poulsen
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameunda kikosi cha wachezaji 32 kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Kenya (Harambee Stars) itakayochezwa Jumanne, Novemba 19 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi hicho kinajumuisha wachezaji 16 walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, na wengine 16 kutoka Future Taifa Stars. Awali kambi ya Future Taifa Stars iliyoanza Novemba 9 mwaka huu na kuvunjwa leo asubuhi ilikuwa na wachezaji 30.

Wachezaji walioitwa ni makipa wanne; Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga), Deogratias Munishi (Yanga) na Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting), Nadir Haroub (Yanga) na Said Moradi (Azam).

Viungo wakabaji ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Shomari Kapombe (AC Cannes, Ufaransa) na Vincent Barnabas anayechezea Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo, Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jonas Mkude (Simba), Ramadhan Singano (Simba), Salum Abubakar (Azam) na William Lucian (Simba).

Viungo washambuliaji ni Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Mrisho Ngasa (Yanga), Mwingi Kazimoto (Markhiya, Qatar) na Simon Msuva (Yanga).

Washambuliaji ni Elias Maguli (Ruvu Shooting), Juma Liuzio (Mtibwa SugarMbwana Samata (TP Mazembe, DRC) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).