STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 15, 2013

SIMBA YATAMBA, LAZIMA LIBOLO IFE JUMAPILI TAIFA



MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ametamba kuwa, kikosi chake kinao uwezo wa kutoa kipigo kwa wapinzani wao, Libolo ya Angola katika pambano lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika litakalofanyika kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Rage amesema kwa kawaida, Simba huwa inabadilika inapocheza katika michuano ya kimataifa hivyo amewataka mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi kuhusu mechi hiyo.
Kauli ya Rage imekuja huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa na hofu na kikosi chao ambacho katika mechi za mwisho za duru la kwanza na mechi tatu za duru la pili walizocheza imekuwa na matokeo yasiyowafurahisha.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Rage alisema mabadiliko ya benchi la ufundi hayawezi kuiathiri Simba katika mechi hiyo kwa vile vijana wake wana ari kubwa ya kuonyesha maajabu.
"Ni kweli baada ya kumuondoa Milovan Cirkovic mfumo wa uchezaji umebadilika, lakini tumejipanga vyema kushinda mechi hiyo na sababu ya kufanya hivyo tunayo,"alisema.
Rage alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na timu inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kutoka Arusha, ambako ilikuwa imeweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.
Kocha Msaidizio wa timu hiyo ambaye pia ni meneja, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alitamba kwamba mashabiki wa soka hawapaswi kuwa na hofu na wajitokeze kwa wingi katika pambano lao la Jumapili wapate raha.
Hata hivyo Julio alisema ni kweli matokeo ya mechi zilizopita hazivutii, lakini soka ndivyo lilivyo na wao wamejipanga hasa baada ya kufanywa marekebisho kwa dosari zilizofanya timu yaoi isitakate katika mechi hizo za Ligi Kuu ikilazimishwa sare mbili mfululizo dhidi ya JKT Ruvu na JKT Oljoro.
Katika hatua nyingine viingilio vya pambano hilo la Wekundu wa Msimbazi na Waangola vimewekwa hadharani ambapo kiingilio cha chini katika mechi kati ya Simba na Libolo kitakuwa sh. 5,000
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, viingilio vingine vitakuwa sh. 10,000 kwa jukwaa la VIP C, sh. 15,000 VIP B na sh.30,000 VIP A.
Kamwaga alisema maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo.

No comments:

Post a Comment