STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 19, 2013

Azam wajipanga kuwalipua Wamorocco kesho Taifa

Kocha wa Azam John Stewart Hall

Kikosi cha Azam kitakachowakabili As FAR -Rabat ya Morocco kesho

KOCHA wa klabu ya Azam ya jijini Dar es Salaam, Stewart Hall, alisema kuwa tayari amewaambia wachezaji wake kutocheza kwa hofu katika mechi yao ya kesho dhidi ya AS FAR ya Morocco itakayokuwa ya kwanza katika hatua ya pili ya mashindano ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wapinzani hao wa Azam walianza kuwasili nchini juzi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayofanyika kuanzia saa 10:00 jioni.
Hall alisema kuwa hadi jana mchana, kikosi chake hakikuwa na majeruhi hivyo anaamini kuwa watafanya vyema na kujiandalia mazingira mazuri ya kusonga mbele.
Akizungumza jana, Hall alisema kuwa anafahamu mechi hiyo itakuwa na ushindani mkali kwa sababu kila upande unataka matokeo mazuri.
"Najua wao wamekuja kusaka matokeo mazuri ugenini ili iwe kazi rahisi nyumbani kwao na sisi tumejipanga kuanza vyema ili tusipate tabu katika mchezo wa marudiano... ni mechi itakayokuwa na ushindani mkali," alisema kocha huyo raia wa England.
Hall aliongeza kwamba wao wanatambua kuwa hatua waliyofika ni ngumu na yenye changamoto huku akisema pia wanakutana na timu yenye uzoefu wa muda mrefu wa kushiriki mashindano ya kimataifa.
"Tunahitaji kuwa makini na kutumia vizuri nafasi tutakazotengeneza ili kupata matokeo bora... nimeshaona baadhi ya mechi zao katika DVD na hivyo tunajua mbinu zao uwanjani," alisema kocha huyo.
Alisema pia hatua waliyoifikia ni nzuri na endapo watasonga mbele, watajiwekea historia kwani klabu hiyo inashiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika inayosimamiwa na kuandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Azam walisonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuzitoa Al Nasri ya Sudan Kusini na Barrack Young Controllers ya Angola.
Hall na kocha mwenzake wa timu ya As FAR Rabat wanatarajiwa kuzungumza na wanahabari asubuhi ya leo kuelezea maandalizi ya kuelekea pambano lao la kesho, wakiwa sambamba na manahodha wa timu hizo.

No comments:

Post a Comment