STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 21, 2013

Aggrey Morris azikatisha tamaa zinazomwania adai ang'oki Azam


Aggrey Morris
BEKI mahiri wa Azam anayeichezea pia timu ya taifa (Taifa Stars), Aggrey Morris, amezikata maini klabu zinazodaiwa kumnyemelea ili zimsajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kusema wazi kuwa, haendi kokote zaidi ya kubaki Azam.
Aidha beki huyo kutoka Zanzibar, alikiri kwamba ligi iliyomalizika wikiendi ilikuwa ngumu na kudai kufurahishwa na namna Azam ilivyozipeleka puta Simba na Yanga kiasi cha kuonekana kama ingetwaa ubingwa msimu huu kabla ya kuteleza.
Akizungumza na MICHARAZO Morris alisema pamoja na kutajwa kuwindwa na klabu kadhaa nchini ili kumsajili, ukweli ni kwamba klabu hizo zinajisumbua bure kwa sababu hana mpango wa kuihama Azam kwa sasa.
Beki huyo wa kati alisema bado ana mkataba na Azam na anauheshimu vilivyo, kadhalika analo deni kubwa kwa klabu hiyo hasa kwa soka la kimataifa hivyo hafikirii kuondoka kirahisi kama inavyotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari.
"Ukweli mimi siendi kokote, mimi ni mchezaji wa Azam nitaendelea kuwa mchezaji wa Azam mpaka mwisho wa mkataba wangu, ni klabu ninayoipenda na ninayoona nina deni kubwa ambalo napaswa kulipwa hasa kwa michuano ya kimataifa," alisema.
Morris ni miongoni mwa wachezaji wanne wa Azam walioshindwa kuitumikia klabu hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo klabu hiyo iliishia kwenye 16 Bora, kutokana na kusimamishwa na uongozi wao kwa tuhuma za Rushwa.
Hata hivyo Morris na wachezaji wenzake, Said Murad, Erasto Nyoni na kipa Deo Munishi 'Dida' walisafishwa na Taasisi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kurejeshwa klabu mwishoni mwa msimu.
Juu ya msimu ulioisha, Morris alisema ulikuwa mgumu na wenye ushindani, huku akidai kufurahishwa na jinsi Azam ilivyozikimbiza Simba na Yanga kiasi cha kukaribia kutwaa ubingwa kabla ya kuteleza na kuiachia Yanga inyakue taji la 24 kilaini.
"Ligi ilikuwa ngumu na huenda msimu ujao ikawa ngumu zaidi kutokana na timu kuonyesha kuimarika kila uchao na hasa kupewa nafasi kwa wachezaji vijana," alisema.

No comments:

Post a Comment