STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, June 5, 2013

Busara Agro Machinery kutambulisha magari mapya mbio za PUMA Rally Juni 14

Wadhamini wa mbio hizo za magari za Juni 14
Na Seleman Msuya
KAMPUNI ya Busara Agro Machinery Tanzania imesema itafungua mashindano ya mbio za magari za jijini Dar es Salaam kwa kutumia magari yao ya Polaris Range RZR ili kuweza kuyatambulisha magari hayo hapa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Mhandisi Oded Kit wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa magari hayo yanatambulika katika mashindano ambapo watakuwa wakifanya maandalizi ya kushiriki mashindano mbalimbali ambayo yatakuwa yakiandaliwa hapa nchini.
Alisema wameshashiriki katika mashindano yaliyopita hivi karibuni ya Arusha Enduro ambapo pia walikuwa kama wafunguzi wa njia ya mashindano lengo likiwa ni kutambulisha magari yao ambayo yamekuwa yakishiriki mashindano ya kimataifa.
Mhandisi Kit alisema Polaris Range RZR ni magari ambayo yanakimbia na imara hivyo wana uhakika kuwa yatafanya vizuri kwa siku za karibuni.
Alisema kampuni yao imedhamiria kuwawezesha madereva ambao wanahitaji kushiriki mashindano ambapo wametoa punguzo la asilimia 30% ya bei ya magari hayo ambayo yanatoka nchini Marekani.
Kit alisema mashindano ya magari yanahitaji maandalizi ya kutosha kuanzia dereva mwenyewe gari, na mahitaji mengine kutokana na ukweli kuwa ni kazi ngumu na ya kuhatarisha maisha.
“Tumesikia kilio chao hivyo tunawaomba waje ili waweze kupata magari imara kwa bei ndogo ambayo tumetoa punguzo la asilimia 30% hivyo tunaamini mtu yoyote akitaka anaweza kununua”, alisema.
Kwa upande wake Fundi Mkuu wa Busara Agro Machinery Denis Gastelleir alisema katika kuonyesha ubora wa magari yao wanatarajia kuwa na magari matatu ambayo yatashiriki katika mashindano ya magari ya PUMA ambayo yatafanyika kuanzia 14 hadi16 mwezi huu kwa kulometa 400 hapa jijini Dar es Salaam.
Alisema magari hayo ambayo yanatokea nchini Marekani yamekuwa yakishiriki katika mashindano mbalimbali kama Dakar Rally na mengine mengi yanayofanyika hapa duniani.
Katika hatua nyingine Kampuni ya mafuta ya PUMA Tanzania imejitolea kudhamini mashindano yam bio za  magari zitakazofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 14 hadi 16.
Hayo yamesemwa na Rais wa Chama Cha Magari Tanzania Nizar Jivan wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na kampuni hiyo ya mafuta ya PUMA pia zipo kampuni zingine ambazo zimejitokeza kudhamini mashindano hayo ambayo yatashirikisha madereva kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika.
Rais huyo alizitaja kampuni tanzu katika kudhamini mashindano hayo kuwa ni pamoja na SUNVIC Express, D.B Shapriya , A TO Z, NIC, CMC, Automobile Ltd, Knight Support, M/S Busara Agro Machinery, New Africa Hotel, Monster Energy Drink, Hari Singh and Sons Ltd, Waljis Travel Bureau and Tazara Reailway.
Jivan alisema hadi sasa ni madereva 25 ambao wamethibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambapo 18 ni Watanzania na 7 wanatoka nje ya nchi ambapo amewataka madereva wengine wenye sifa wajitokeze ila.
“Tarehe 14 hadi 16 tunatarajia kuwa na mashindano ya kukimbiza magari ambayo yatakuwa ni ya kilometa 400 na yatafanyika hapa Dar es Salaam ambapo tutatumia barabara mbalimbali tukianzia Tazara”, alisema.
Rais huyo alisema katika mashindano hayo kutakuwa na magari mbalimbali kama Subaru Impreza R14, Mistubish Evolution X, Subaru Impreza N12, Mistubishiu Evolution 8, Subaru Impreza MY04, Subaru Impreza MY03, Mistubish Evolution IX, Subaru Impreza MY06, Subaru LEGACY, Mistubish Galant VR4, Toyota CelicaGT-4, Mistubish EvolutionIV, Subaru Impreza GC8, Range Rover, Toyota Land Cruser, VW Beetle, Nissan 240Z na Toyota Spinter.
Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya PUMA ambao ndio wadhamini wa kuu wa  mashindano hayo Philippe Consaletti alisema wao wamejipanga kuendelea kudhamini mashindano hayo kama moja ya sehemu ya faida yao ambayo wanaipata hapa nchini.
Consaletti alisema katika kutekeleza hilo wanatarajia kudhamini mashindano ya mwaka ujao ambapo wameahidi kuwa yatafanyika mkoani Arusha wakati ukifika.
Kwa upande wake Kamanda wa Usalama Barabarani Kamishna Mohammed Mpinga amewahakikishia madereva na raia ambao watakuwa katika maeneo ambayo magari yatapita kuwa usalama utakuwepo.
Mpinga aliwataka raia kuzingatia na kufuata utaratibu ambao utakuwa unatumika ili kuepusha kero mbalimbali ambazo zinaweza kutokea.

No comments:

Post a Comment