Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima |
IGP, Said Mwema |
JUMLA ya askari wa 114 wa Jeshi la Polisi wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa maadili ya kazi zao na baadhi yao wakiwa wamefikishwa mahakamani katika kipindi cha mwaka 2007-2010.
Takwimu hizi zimefichuliwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima wakati akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Jaku Hashim Ayoub.
Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kudhibiti vitendo vya baadhi ya askari kuwabambikia kesi raia kinyume na misingi ya haki za binadamu.
Pia alitaka kujua serikali imewachukulia hatua gani za kinidhamu na kisheria askari waliojihusisha na vitendo hivyo ili iwe fundisho kwa askari wengine.
Akijibu, Silima alisema serikali ina mikakati ya kukabiliana na kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora pamoja na vitendo vya baadhi ya askari kuwabambikia kesi na kuwatishia raia ili wasifuatilie kesi zao vituoni.
“Kuanzia mwaka 2007 hadi 2010 jumla ya askari 114 wamefukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa maadili na maadhi yao wamefikishwa mahakamani” alisema.
Hata hivyo, alisema mafanikio ya jeshi la polisi yanategemea upatikanaji wa taarifa za matukio hayo kutoka kwa wananchi ambao wanatendewa vitendo hivyo na baadhi ya askari ambao siyo waaminifu.
Hivi karibuni askari karibu 10 nchini waliripotiwa kutimuliwa kazi kwa makosa mbalimbali ikiwemo wale waliokuwa wakitumia fuvu la mtu kuwapakazia kesi wananchi katika mkoa wa Morogoro.
No comments:
Post a Comment