BEKI wa timu ya taifa ya Hispania, Jordi Alba amejishangaa kwa kuweza kufunga mabao mawili na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi baada ya kuisaidia timu yake kushinda 3-0 dhidi ya Nigeria katika mechi yao ya mwisho ya makundi ya Kombe la Mabingwa wa Mabara 2013 juzi usiku.
Mlinzi huyo wa kushoto wa Barcelona alifunga goli kali la juhudi binafsi mapema kipindi cha kwanza kabla ya kutupia la tatu baada ya kukimbia kutokea katikati ya uwanja na kumpiga chenga kipa Vincent Enyeama katika dakika za mwisho.
"Si kawaida kwangu kufunga magoli mawili katika mechi moja," Alba aliwaambia waandishi wa habari. "Nadhani hii ni mara ya kwanza.
"Hii ni mpya kwangu, kwa sababu, kama ulivyosema, mara nyingi tuzo hii (ya mchezaji bora wa mechi) hupewa washambuliaji au wale walio mbele katika mechi kubwa. Najivunia kupata tuzo hii."
Kocha Vicente del Bosque alilalamikia hali ya hewa mjini Fortaleza Jumapili jioni, na Alba alikiri kwamba joto limekuwa likiziathiri timu katika michuano hiyo.
"Tulisikia joto katika mechi nzima, ilikuwa ni joto sana," aliendelea. "Miguu yako inaungua... Lakini iko hivyo kwa timu zote."
Hispania sasa itacheza dhidi ya Italia katika nusu fainali katika mechi ambayo ni kama marudio ya fainali ya Euro 2012, ambayo Hispania ilishinda 4-0, lakini Alba amesisitiza kwamba timu yake ni lazima iwe katika kiwango cha juu ili kuishinda timu ya kocha Cesare Prandelli.
"Dhidi ya timu kama Italia hujui nini kitatokea," alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24. "Wanajipanga vyema nyuma na wanajua kukaa na mpira.
"Watakuwa wagumu kwetu, kama ambavyo wamekuwa kila siku. Tunapaswa kudumusha staili yetu ya kucheza na kutoruhusu magoli nyuma."
No comments:
Post a Comment