MUIGIZAJI wa kike wa filamu nchini, Leah Mussa 'Shasta' amefuata mkondo wa shoga zake Shilole na Snura kwa kujitosa kwenye muziki akikamilisha wimbo wake wa kwanza uitwao 'Utamu wa Penzi' ambao amemshirikisha Hamis Mbizo 'H-Mbizo'.
Akizungumza na MICHARAZO Shasta alisema wimbo huo upo hatua ya mwisho kabla ya kukamilika akiwa ameurekodia katika studio za prodyuza More Fire aliyetengeneza wimbo wa Snura uitwao 'Majanga'.
Alisema kuingia kwake kwenye muziki siyo kwa kubahatisha kwani tangu utotoni alikuwa akijishughulisha na muziki akiimba kanisani na shuleni na mpaka sasa yeye ni mwalimu wa muziki na anaimba kwaya ya kanisa lake la Sabato, ila hakuifanya kazi hiyo kibiashara kutokana na kutingwa na majukumu ya uigizaji wa filamu.
"Wengine wanaweza kuhisi landa nimevamia fani ya uimbaji, hapana mimi ni mwanamuziki kamili nikianza kuimba kanisani na shuleni tangu nikiwa mdogo na hata sasa naimba kwaya kanisani, ila kwa vile nataka kuwaonyesha wengine kwamba watu tuna vipaji zaidi ya kimoja ndiyo maana nimeamua kutoka na wimbo huo wa 'Utamu wa Penzi' kisha kufuatiwa na nyimbo nyingine," alisema Shasta.
Nyota huyo wa filamu ya 'Kisasi cha Mzimu', 'Julia', 'Deception', 'Ongwana', Pete ya Ajabu na nyingine, alisema mara baada ya kuachia hewani wimbo huo klabla ya kuanza kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani unaoanza wiki mbili zijazo ataanza mipango ya kukamilisha video yake kabla ya kutoa kazi mpya hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment