Kaimu Kamanda Mkuu wa Polisi Mkoa wa Njombe, Focus Malengo |
WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamewaua kwa kuwapiga risasi walinzi wawili wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Makambako Security Guard katika mji mdogo wa Makambako mkoani Njombe.
Tukio hilo lilitokea jana saa 12:30 asubuhi baada ya watu hao kuvamia kituo cha kuuzia mafuta cha Oryx cha mjini hapa.
Walinzi waliouawa wametajwa kuwa ni Chesco Mpogole (30) na Damas Sanga (28), wakazi wa Ubena na Uhuru mjini hapa.
Mbali na watu hao kuuawa, pia majambazi hayo yamemjeruhi vibaya Meneja wa Kituo hicho, Jonas Msengi (43), mkazi wa Mji Mwema ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Ilembula kwa matibabu.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Focus Malengo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kamanda Malengo alisema majambazi hayo yalivamia kituo hicho kwa kutumia usafiri wa pikipiki na kujifanya wateja wa kununua mafuta.
“Lakini wakiwa tayari wameuziwa mafuta ya Sh. 5,000, yalitoa noti ya Sh. 10,000, hivyo mhudumu aliyewahudumia Ibrahim Manga, alikwenda kwa mwenzake Mwanaidi Kalinga (32) kwa ajili ya kufuata chenji,” alisema Kamanda Malengo.
Aliongeza kuwa wakati jambazi moja likisubiria chenji, mwingine aliwafuata walinzi hao na kuwashambulia kwa kuwapiga risasi na kusababisha vifo vyao papo hapo.
Kamanda Malengo alisema baada ya kufanya mauaji hayo, majambazi hayo yalimfuata Meneja Msengi, ambaye wakati huo alikuwa akiingia ofisini kwake na kuanza kumshambulia.
“Lakini pia majambazi hayo yalipora kiasi cha kati ya Shilingi milioni sita na saba kwa taarifa za awali kwani wamiliki wa kituo hiki wanaendelea kufanya hesabu zao,” alisema Kamanda Malengo.
No comments:
Post a Comment