BAADA ya kuwanyakua wachezaji wawili kwa mpigo Cosmas Lewis toka Azam na Elias Maguli kutoka Prisons-Mbeya, maafande wa Ruvu Shooting imefanikiwa kumnasa mshambuliaji mwingine nyota, Jerome Lembeli kutoka kwa timu iliyopanda daraja ya Ashanti United.
Lembeni aliyewahi kuichezea Moro United na kutamba kwenye timu ya taifa ya vijana U17 ametua Ruvu kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kusainishwa juzi na uongozi wa klabu hiyo.
Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire alisema kunyakuliwa kwa mshambuliaji huyo aliyeifungia Ashanti mabao 16 wakati wakiirejesha ligi kuu kuna kusuidia kuimarisha safu ya ushambuliaji wa timu yake ambayo msimu uliopita haikuwa na bahati hasa ilipompoteza Abdallah Seif Karihe aliyepo Azam.
Bwire alisema rekodi za kuvutia za Lembeli ndizo zilizowafanya wamsajili katika muendelezo wao wa kuimarisha kikosi chao kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu 2013-2014.
Limbeli ndiye aliyeifungia Tanzania katika michuano ya U17 bao pekee walipotwaa ubingwa wa Dunia na pia alikuwa mfungaji wa pili katika michuano ya U17 ya Copa Coca Cola iliyofanyika Afrika Kusini akifunga mabao matano moja pungufu la mfungaji bora toka Nigeria.
Pia amekuwa akitoa mchango mkubwa katika timu za taifa za Serengeti Boys na ilemya U20 tangu alipoanza kuitwa, mbali na kuichezea timu ya taifa mara kadhaa ilipokuwa chini ya kocha Marcio Maximo kabla ya kurejea kwao Brazili.
"Kwa sifa hizo katika kufumania nyavu tumeona ni vyema tuwe naye na tumemsajili kwa mkataba wa miaka miwili tukiamini atatoa mchango mkubwa kwa kikosi cha timu yetu ambacho kimepania msimu ujao iwe tishio baada ya msimu huu kuteleza," alisema Bwire.
Klabu mbalimbali za soka kwa sasa zipo katika harakati za kuimarisha vikosi vyao baada ya kumalizika kwa msimu wa 2012-2013 ambapo ilishuhudiwa timu za majeshi zikichechemea na kuziacha timu za kiraia zikitamba ambapo Yanga ilikuwa bingwa, ikifuatiwa na Azam, Simba,Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Coastal Union zilizomaliza kwenyue Sita Bora.
No comments:
Post a Comment