STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 1, 2013

CUF yajipanga kuchukua hatua dhidi ya Jeshi, Polisi

 
http://zanzibardaima.files.wordpress.com/2013/01/lipumba1.jpg?w=640
Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kinawasilisha na mawakili wake na asasi za haki za binadamu kujua hatua za kisheria kuchukua dhidi ya  askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa madai ya kutekwa na kuteswa Naibu Mkurugenzi wa CUF Taifa, Shaweji Mketo, na viongozi wengine wa chama hicho Mkoa wa Mtwara.
Mpango huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wake wa Taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba wakati akiongea na waandishi wa habari.

Prof. Lipumba alisema pia chama hicho kinawasiliana na mawakili hao kujua hatua za kisheria za kuch
ukua dhidi ya Jeshi la Polisi kwa madai ya kuwabambikia kesi viongozi hao  ambao kimedai walikamatwa na kupigwa na askari wa JWTZ katika kambi yao ya Naliendele.
Alisema pia wanawasiliana na asasi za kiraia zinazoshughulikia haki za binadamu na haki za wanawake kumsaidia kisaikolojia mwanamke anayedaiwa kubakwa na askari wa JWTZ mkoani humo na kufikishwa mahakamani.

Lipumba aliwataja viongozi wengine wa CUF waliodaiwa kutekwa na kuteswa kambini Juni 28, mwaka huu kuwa ni Salum Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa CUF Mtwara Mjini,Ismail Jamal Mwenyekiti wa CUF Mtwara vijijini.

Wengine ni Mwenyekiti wa Vijana Mtwara mjini, Ismail Njalu, Katibu wa CUF Mtwara mjini, Said Kulaga na Kashindye Kalungwana ambaye ni dereva wa jeshi hilo makao makuu.

Alidai viongozi hao baada ya kutekwa na askari wa JWTZ walivuliwa nguo zote na kulazwa kifudifudi, kumwagiwa maji ya baridi na kupakwa chumvi kisha kuanza kupigwa usiku kucha kwa kutumia mikanda ya jeshi, ngumi, mateke na fimbo maalum za ngozi za wanyama na miti maalum.

Alisema viongozi hao wakiwa njia kurejea Mtwara Mjini wakitokea Msimbati magari mawili ya jeshi yaliziba barabara baada ya kuliona gari la CUF  na wanajeshi walianza kuwashusha na kuwapiga kisha kuwarusha kwenye karandinga lao.

Alisema baadaye walipelekwa katika kambi ya Naliendele kabla ya kuachiwa saa 5:00 usiku na kukabidhiwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.

“Kwa bahati mbaya Mketo alipigwa sana katika ubavu wake wa kulia ambao amewahi kufanyiwa operesheni kubwa miezi kadhaa iliyopita,. 

Alipoona anapigwa sana eneo hilo akaona awaombe askari wampige maeneo mengine lakini eneo hilo wamhurumie, kusikia vile askari wale walimgeuza kwa nguvu na kuanza kumpiga mateke ya nguvu zaidi katika eneo lile hadi alipoteza fahamu,”alisema.
Alisema Mketo alipozinduka Juni 28, mwaka huu  alijikuta ana dripu na hakuelewa ni ya nini na baadaye wanajeshi waliitoa.

Profesa Lipumba alisema tukio la utesaji raia ndani ya kambi ya jeshi ikiliunganishwa na matukio mengine kama ya utesaji wa Dk.Stephen Ulimboka , kutekwa nyara kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, kulipuliwa bomu katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kunadhihirisha hatua za awali za kusambaratika kwa dola.

Msemaji wa JWTZ, Kapambala Mgawe, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa askari wa jeshi lake,  alisema suala hilo linatiwa chumvi na wanasiasa kwasababu kiutaratibu anayetekwa ni adui hivyo raia wa Tanzania hawezi kutekwa na wanajeshi.

Mgawe alisema tuhuma zinazoelekezwa kwa wanajeshi zina lengo la kutaka kulichafua jeshi hilo ili lisifanye kazi yake kwasababu vipo vipengele vya kisheria vinavyoruhusu askari wa JWTZ kuliingilia kati kudumisha amani kunapotokea Jeshi la Polisi limezidiwa.

Alisema katika kipindi hiki ambacho kuna vurugu nyingi zinajitokeza katika nchini jeshi litakapokuwa linachukua hatua ya kudhibiti yatesemwa mengi ikiwamo askari kuhusishwa na vitendo vya ubakaji.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment