Kocha Arsene Wenger |
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba kuwa hatarajii kumsajili Cesc Fabregas katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi kwani kiungo huyo wa timu ya taifa ya Hispania ameamua kubaki kwa "mwaka mmoja zaidi " kwenye klabu yake ya Barcelona.
Arsenal wamesisitiza kuwapo kwa kipengele kinachowaruhusu kumnunua tena Fabregas kwa paundi za England milioni 25 ambacho kiliwekwa wakati wa mkataba wao wa kumuuza Mhispania huyo kwa Barca miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo, licha ya Manchester United kujaribu kumtwaa kwa kuwasilisha ofa ya euro milioni 30 Jumatatu iliyopita, Mfaransa Wenger anaamini kwamba wao hawahitaji kutuma ofa yoyote kwa nia ya kumzuia nahodha wao huyo wa zamani kwenda Man U.
Iliripotiwa mwishoni mwa mwezi uliopita kuwa Wenger amekuwa akiwasiliana kila mara na nahodha wake huyo wa zamani, na sasa amedai kuwa anafahamu msimamo wa Mhispania huyo kuhusiana na hatma yake msimu ujao.
"Hivi sasa, Fabregas ameamua kubaki Barcelona kwa mwaka mmoja zaidi," Wenger aliwaambia waandishi wa habari.
Nahodha huyo wa zamani wa Arsenal amekuwa akihaha kupata nafasi ya uhakika katika kikosi cha kwanza tangu arejee katika timu yake ya utotoni lakini kuondoka kwa Thiago Alcantara kwenda Bayern Munich kunamaanisha kuwa sasa ana nafasi kubwa ya kucheza katika kiungo cha kocha Tito Vilanova.
Vilanova alisisitiza mwanzoni mwa wiki hii kwamba kiungo huyo mwenye miaka 26 anataka kubaki Barca na kuigania namba.
Alisema: "Natambua kwamba tumepokea ofa kadhaa kutoka klabu nyingine. Nilizungumza naye na ameniambia anataka kubaki.
"Cesc hafikirii kuhamia katika klabu nyingine. Anajua kwamba ushindani hapa ni mkubwa. Ndoto zake ni kuona anafanikiwa akiwa hapa."
Katika hatua nyingine kocha huyo amesema klabu yake inamudu mshahara wa kumlipa mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney anayetajwa kutaka kuhama Old Trafford licha ya klabu kudai HAUZWI.
Wenger alisema kama mchezaji huyo ataamua kukubali kutua kwao hawatakuwa na tabu ya kumlipa mshahara ambao kwa wiki hulipwa pauni 250,000.
"Rooney ana mkataba na amebakisha miaka miwili uishe, hivyo ni Man U wenye maamuzi. Lakini hatutakuwa na shida kulipa mshahara wa Rooney." alinukuliwa kocha huyo kutoka Ufaransa.
No comments:
Post a Comment