STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 19, 2013

Salha atua King's Modern Taarab


MUIMBAJI wa zamani wa kundi la Dar Modern Salha Abdallah 'Salha wa Hammer' aliyetimuliwa katika kundi hilo kwa kutoa wimbo binafsi na mumewe, amejiunga na la King's Modern Taarab na ameanza kuijifua kwa ajili ya maonyesho ya sikukuu ya Idd el Fitri.
Salha aliyetamba na vibao kadhaa akiwa na Dar Modern ukiwamo utunzi wake uliobeba jina la albamu ya 'Nauvua Ushoga' amelamba ajira King's Modern Julai 4 mwaka huu na anaendelea kujifua nao kwa ajili shoo za Idd na maandalizi ya albamu mpya ya kundi hilo.
Akizungumza na MICHARAZO, Salha alisema amesaini mkataba wa kulifanyia kazi kundi hilo linalotamba na kibwagizo cha 'Kijoka chazima taa' na hakuona sababu ya kuvunga huku akiwa ameshatimuliwa katika kundi lake la zamani.
"Baada ya kutemeshwa mzigo Dar Modern hivi karibuni, kundi la King's Modern limenifuata na kuniomba kujiunga nalo na kwa sasa mimi ni muimbaji wa kundi hilo, tunajiandaa kwa shoo za sikukuu ya Idd," alisema Salha.
Alisema hana cha kuahidi kwa mashabiki wa kundi hilo lakini wajiandae kupata burudani kabambe akishirikiana na wanamuziki wenzake ambao wamempokea kwa mikono miwili.
Uongozi wa Dar Modern unadaiwa kumtimua Salha baada ya muimbaji huyo na mumewe kutoa wimbo wa 'Mapenzi Matamu' (Wapendanao) kinyume na utaratibu uliopo ndani ya kundi hilo, japo Salha alilia kwamba hakutendewa haki kwa vile aliyeimba naye katika kazi hiyo ni mumewe na siyo kundi au msanii mwingine wa nje.

No comments:

Post a Comment