Ozil na baba yake |
Mesut Ozil |
MADRID, Hispania
BABA wa Mesut Ozil, Mustafa, ametishia kuchukua hatua za kisheria kufuatia taarifa za katika vyombo vya habari nchini Hispania kudai kwamba kiungo huyo Mjerumani alikuwa akiathiriwa kipaji chake na matatizo ya nje ya uwanja wakati akiwa Real Madrid.
Mapema wiki hii, gazeti la Hispania liitwalo ABC, ambalo lina mahusiano na rais wa Real, Florentino Perez, liliripoti kuwa rais huyo wa Madrid anaamini kwamba Ozil "hakuwa vizuri kiweledi na alikuwa akichanganywa na wanawake na maisha ya kujirusha usiku".
Lakini baba wa kiungo huyo Mjerumani amejia juu tuhuma hizo akisema Perez anajaribu kumfanya kiungo huyo aliyetua Arsenal kuwa mbuzi wa kafara.
"Kwa sababu tu ana pesa nyingi haimaanishi kwamba yeye ni mtu wa heshima," baba wa Ozil alikaririwa na gazeti la Bild. "Na Perez si mtu wa heshima.
"Mesut anatumiwa kama mbuzi wa kafara sasa lakini baba yake nipo. Nitaingia mchezoni. Tutatetea upande wetu kisheria.
"Kama Mesut alikuwa na maisha yasiyozingatia weledi Madrid, kwanini sasa alikuwa akichezeshwa kila siku? Wanataka kumlaumu sasa kwa vile mashabiki na wachezaji wenzake wamekasirika (kuuzwa kwake)."
Ozil, ambaye alifunga ama kutoa pasi ya magoli 108 katika mechi 159 akiwa na Madrid, alikamilisha uhamisho wa aina yake katika siku ya mwisho na kutua Arsenal kwa ada ya paundi milioni 40, jambo lililowakera wachezaji wenzake wengi akiwamo Cristiano Ronaldo.
No comments:
Post a Comment