STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 13, 2013

Simba kamili gado 'kuiua' Mtibwa kesho, Owino, Dhaira watua

Joseph Owino
KLABU ya soka ya Simba imekamilika tayari kulipa kisasi kwa Mtibwa Sugar kesho katika pambano lao la Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya nyota wao wa kimataifa kutoka Uganda, Abel Dhaira na beki Joseph Owino kuwasili kikosini.

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliliambia MICHARAZO kuwa, kikosi chao kipo 'kamili gado' kambini na kesho kitashuka dimba la Taifa, Dar es Salaam kwa nia ya kulipa kisasi kwa Mtibwa waliowanyuka na kuzoa pointi zote sita katika mechi mbili za msimu uliopita.

Kamwaga alisema benchi lao la ufundi limewahakikishia wachezaji wote wapo fiti kukiwa hakuna majeruhi na la furaha zaidi ni kurejea kwa mastaa wao wa Uganda, kipa Dhaira na beki Owino waliokuwa wameenda kwao kwa matatizo ya kifamilia.

"Tunashukuru kambi yetu ipo fiti na kwamba kikosi kimekamilika baada ya nyota wetu kutoka Uganda kutua nchini tayari kwa vita ya kesho, lengo likiwa kulipa kisasi dhidi ya Mtibwa sambamba na kuzoa pointi zitakazotuweka pazuri katika msimamo wa ligi," alisema.

Kamwaga alisema Simba inafahamu mechi ya kesho itakuwa ngumu na yenye upinzani mkali, lakini wamehakikishwa na benchi lao la ufundi pamoja na wachezaji wenye ari kuwa ushindi ni lazima Taifa kabla ya kusubiri mechi yao ijayo ya siku ya Jumatano dhidi ya Mgambo JKT.

Simba iliyoanza ligi hiyo kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino Rangers kisha kuifunga JKT Oljoro, ililala bao 1-0 jijini Dar es Salaam katika mechi yao ya pili dhidi ya mabingwa hao wa Tanzania  wa 1999 na 2000 baada ya awali kufungwa mabao 2-0 mjini Morogoro.

Baadhi ya nyota wa Mtibwa Sugar kama Salum Sued 'Kussi' na Salvatory Ntebe wametamba kuwa wamekuja  Dar kwa nia moja ya kuzoa pointi tatu pamoja na kuendeleza ubabe kwa vijana wa Msimbazi, licha ya kukiri litakuwa pambano la 'kufa mtu'.

Mtibwa kama ilivyo Simba na klabu nyingine tano zinazokamata nafasi ya pili nyuma ya JKT Ruvu ina pointi nne zilizotokana na sare ya 1-1 dhidi ya Azam na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya ndugu zao wa Kagera Sugar ambao kesho wapo Kagera kuumana na Azam.

Mechi nyingine za kesho ni kati ya Mbeya City na Yanga zitakazoumana uwanja wa Sokoine Mbeya, JKT Ruvu itakayokuwa wageni wa Ashanti Utd uwanja wa Chamazi, Coastal Union kuialika Prisons-Mbeya na JKT Oljoro itakayoikaribisha Rhino Rangers ya Tabora.

No comments:

Post a Comment