STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, November 29, 2013

Kili Stars yaanza kwa sare dhidi ya Chipolopolo, Uganda kuanza kutetea taji

Na Somoe Ng'itu, Nairobi
KILIMANJARO Stars imeanza michuano ya Kombe la Chalenji kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopo) ambayo nchi yao inashika nafasi ya 72 katika viwango vya Fifa duniani vilivyotangazwa jana.
Timu hiyo ya Tanzania Bara ambayo nyota wake pamoja wa Zanzibar Heroes huunda timu ya Taifa (Taifa Stars), ilikuwa ya kwanza kufungwa kipindi cha kwanza kabla ya kipindi cha pili kusawazisha.
Chipolopolo inashiriki michuano  inayoandaliwa na Shirikisho la Sola la nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kama timu alikwa.
Mechi hiyo ya Kundi B, ilianza kwa dakika ya pili ya mchezo, mshambuliaji Elias Maguli kupenyeza pasi safi kwa Salum Abubakar 'Sure Boy' lakini kipa Nsabata Toaster wa Zambia alipangua kishujaa shuti la kiungo huyo wa Azam FC.
Katika dakika ya 22, winga hatari mwenye mabao sita Yanga msimu huu, Mrisho Ngasa, alikokota mpira hadi ndani ya boksi la Zambia, lakini akapiga shuti nje ya lango. Katika mchezo wa mwisho dhidi ya Zambia uliokuwa wa kirafiki jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana, Ngasa aliifungia Timu ya Taifa (Taifa Stars) bao pekee katika ushindi wa 1-0.
Ngasa alipiga shuti pia katika dakika ya saba ya mchezo wa jana, lakini lilidakwa na kipa Toaster.
Zambia walipata bao katika dakika ya 41 lililodumu kipindi chote cha kwanza kupitia kwa Ronald Kampamba aliyemalizia krosi murua ya mkongwe, Felix Katongo.
Kili Stars walitengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza lakini waliponzwa na umaliziaji duni huku Zambia wakipiga mpira wa pasi fupi fupi laki jitihada zao zilikwamishwa na kipa Ivo Mapunda aliyeokoa michomo mingi langoni.
Beki Said Morad aliisawazishia Tanzania Bara dakika tatu baada ya kipindi cha pili kuanza akiunganishwa kwa kichwa kona safi iliyochongwa na Sure Boy ambaye alitangazwa mchezaji bora wa mchezo huo.
Ngasa alitaka kusahihisha makosa alipoachia shuti kali lakini likapanguliwa kishujaa na kipa Toaster.
Dakika ya 82 Haroun Chanongo alipiga shuti likadakwa.
Kwa matokeo hayo Burundi anaongoza Kundi B baada ya kuilaza Somalia kwa mabao 2-0 katika mechi ya awali iliyochezwa mchana kwenye uwanja huo.
Michuano hiyo itaendelea leo saa 8:00 mchana kwa Sudan kucheza dhidi ya Eritrea, mchezo utakaofuatwa na Uganda dhidi ya Rwanda saa 10:00 alasiri kwenye Uwanja wa Machakos.
Jumamosi Zanzibar Heroes itaumana na Ethiopia kwenye Uwanja wa Nyayo katika mchezo wa utangulizi na baadaye Sudan Kusini itapambana na Kenya kwenye uwanja huo huo.
Kili Stars itacheza mchezo wa pili dhidi ya Somalia Jumapili kuanzia saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Nyayo wakati Zambia itamenyana na Burundi kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 10:00 jioni siku hiyo.
Kili Stars iliwachezesha: Ivo Mapunda, Erasto Nyoni, Said Morad, Kelvin Yondani, Himid Mao, Frank Domayo, Salum Abubakar 'Sure Boy'/ Ramadhani Singano 'Messi' (dk 88), Hassan Dilunga/ Athuman Idd 'Chuji' (dk 85), Mrisho Ngasa, Elias Maguli/ Haroun Chanongo (dk 72) na Amri Kiemba.
Zambia: Nsabata Toaster, Bronson Chama, Jimmy Chisenga/ Kabaso Chongo (dk 67), Christophe Munthali, Rodrick Kabwe, Stanley Nshimbi/ Alex Nyonga (dk 57), Sydney Kalume, Kondwani Mtonga, Felix Katongo/ Salalani Phiri (dk 73), Ronald Kampamba na Festus Ndewe.

No comments:

Post a Comment