STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 7, 2013

Kili Stars hiyoo nusu fainali ya Chalenji, Ivo Shujaa

Mashujaa wetu Kilimanjaro Stars waliotinga nusu fainali za Chalenji
TIMU ya Kilimanjaro Stars imefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Chalenji baada ya kuwavua taji waliokuwa watetezi wa michuano hiyo Uganda The Cranes kwa mikwaju ya penati 3-2 baada ya kumaliza muda wa kawaida wakifungana mabao 2-2, Shujaa akiwa Ivo Mapunda aliyedaka penati mbili.
Kwa ushindi huo Stars sasa itavaana na wenyeji wao Kenya, Harambee Stars ambayo jioni hii nayo imepoata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rwanda 'Amavubhi' katika robo fainali ya pili.
Katika pambano la Kili Stars dhidi ya Uganda, lililochezwa kwenye uwanja wa Manispaa ya Mombasa, Kenya, Uganda ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza likifungwa na Daniel Sserunkuma katika dakika ya 16 akimalizia krosi ya Hamis Kiiza, kabla ya Mrisho Ngassa kusawazisha dakika mbili baadaye.
Baada ya bao hilo Stars walizidi kucharuka na kuliandama lango la The Cranes kabla ya Ngassa kuwanyamazisha waganda kwa kufunga bao la pili dakika ya 39, matokeo yaliyodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Kili Stars inayofundishwa na Kim Poulsen, raia wa Denmark, ilipata pigo baada ya kiungo wake Salum Abubakar 'Sure Boy' kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kucheza rafu, ambapo nafasi hiyo iliwapa nguvu Uganda kupata bao la kusawazisha kupitia Martin Mpuga matokeo yaliyodumu hadi mwisho.
Ndipo ikafuata changamoto ya penati na Tanzania kufanikiwa kupata mikwaju mitatu kupitia kwa Amri Kiemba, Athuman Idd 'Chuji' na nahodha Kelvin Yondani, huku Uganda wakipata  kupitia kwa Emmaneul Okwi na Hamis Kiiza.
Waliokosa kwa Kili Stars ni Erasto Nyoni na Mbwana Samatta aliyekuwa nyota wa mchezo huo wa leo, huku Godfrey Walusimbi, Khalis Alucho na Sserunkuma walikosa baada ya kipa Ivo Mapunda kuonyesha ushujaa kwa kuokoa mikwaju yao na kuivusha Kili Stars nusu fainali na ikilipa kisasi kwa Uganda.
Kenya nayo ilifuatia baadaye uwanjani na kupata ushindi wa bao 1-0 na hivyo kujikuta uso kwa uso na Kili Stars ambayo mwaka uliopita ilishika nafasi ya nne kwa kufungwa na ndugu zao Zanzibar Heroes ambato safari hii wametoilewa hatua ya makundi.

No comments:

Post a Comment