STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 29, 2014

Cheka kutoa 'hogo' leo, akijianda kuwania ubingwa wa dunia

WAKATI Francis Cheka akitarajiwa kutoa 'hogo' alililofungwa kwenye mkono wake wa kulia leo, bondia huyo sasa atapigana na mpinzani wake kutoka Russia, Valery Brudov kuwania ubingwa wa dunia wa WBF uzito wa Lightheavy.
Cheka aliumia mkono huo katika maandalizi ya pambano lake dhidi ya Brudov ambalo awali lilipangwa kufanyika Februari 8, lakini sasa limesogezwa mbele hadi Machi Mosi.
"Cheka anatarajiwa kutolewa plasta gumu (P.O.P) mkononi na kuangaliwa hali yake na daktari kesho (leo) na kama maendeleo yake ni mazuri ataanza kujifua kwa ajili ya pigano lake Machi Mosi," alisema Msangi.
Mratibu wa pambano hilo, Juma 'Jay' Msangi' aliiambia MICHARAZO kuwa, Cheka anatarajiwa kutolewa 'hogo' hilo leo kabla ya kuanza maandalizi ili kujiweka fiti kwa pambano hilo litakalofanyika ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam.
Msangi alisema tofauti na ilivyokuwa awali, pambano la Cheka na Brudov sasa litakuwa la kuwania ubingwa wa dunia uzani wa kilo 82 (Light Heavy Weight) na imani yake bingwa huyo wa IBF Afrika atawatoa kimasomaso Watanzania.
Aidha, mratibu huyo alisema mapambano mengine yaliyokuwa yamepangwa kuchezwa Februari 8 yatafanyika kama ilivyopangwa na sasa pambano la bondia Francis Miyeyusho na Victor Chornous kutoka Ukraine ndilo litakalokuwa pambano kuu siku hiyo.
Msangi alisema licha ya pambano la Miyeyusho, bingwa wa kimataifa wa UBO uzito wa Bantam pia siku hiyo kutakuwa na michezo mingine kadhaa ya utangulizi likiwemo la Mohamed Matumla dhidi ya Nassib Ramadhan.
Mabondia hao wawili walipigana hivi karibuni kuwania pikipiki na Matumla ambaye ni mtoto wa bingwa wa zamani wa WBU, Rashid Matumla 'Snake Man', aliibuka kidedea dhidi ya mpinzani wake na kunyakua 'bodaboda' hiyo.

No comments:

Post a Comment