STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, January 18, 2014

Coastal yalazimishwa sare na Seeb Oman


Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, leo wametoka suluhu tasa dhidi ya Seeb SC inayoshiriki ligi kuu ya Oman.
Mechi ya leo ambayo ni ya kirafiki imeisha kwa matokeo ya 0-0 ambayo inakuwa mechi ya nne tangu kuwasili nchini hapa Januari 9, kwa ziara ya wiki mbili kujiandaa na ligi mzunguko wa pili Tanzania Bara.
Coastal Union, imeonyesha uhai katika kipindi cha pili ambapo kipindi cha kwanza walishindwa kuonyesha makeke yao baada ya wachezaji wa Seeb, kujazana katikati hali iliyowafanya Wagosi kushindwa kumiliki mpira.
Aidha, golikipa wa Wagosi, Shaaban Kado alipoiona kasoro hiyo akawa anatumia muda mwingi kupiga mipira katikati kila inapomjia kwa lengo la kuamsha mashambulizi ili viungo wake wachangamke.
Kipindi cha kwanza kiliisha timu zote kizitoka vichwa chini kutokana na kukosa nafasi za kuonyeshana uwezo waliofundishwa na walimu wao.
Kipindi cha pili Seeb Club, walifanya mabadiliko kwa kutoa wachezaji wawili wa ndani na mlinda mlango. Coastal Union waliendelea kucheza bila kufanya mabadiliko.
Katika dakika za awali kipindi cha pili Seeb walionyesha uhai na kulisumbua sana lango la Wagosi, lakini kufuli za Juma Nyoso na Othman Tamim ziliendelea kuwa imara kuulinda mlango wa Shaaban Kado.
Aidha ilipofika dakika ya 76, kocha Yusuf Chipo alifanya mabadiliko ya haraka haraka kwa kutoa wachezaji wane na kuingiza wane ndani ya dakika 15 zilizosalia.
Alianza kutoka Othman Tamim akaingia Abdi Banda, baadae akatoka Danny Lyanga akaingia Mohammed Miraji. Halafu zikiwa zimesalia dakika chache mchezo kuisha alitoka Atupele Green akaingia Suleiman Kassim Selembe, halafu akamalizia mabadiliko kwa kumuingiza Abdullah Othman ‘Ustadh’ akatoka Yayo Kato.
Listi ya leo ilikuwa: Shaaban Kado, Hamadi Juma, Othman Tamim, Juma Said ‘Nyoso’, Mbwana Kibacha, Jerry Santo, Ally Nassor ‘Ufudu’, Danny Lyanga, Atupele Green, Haruna Moshi ‘Boban’, na Yayo Kato.
Coastal Union tangu iwasili Oman imeshacheza mechi nne, imeshinda mechi mbili kati ya Oman Club na Al Mussannah kwa mabao 2-0 kila mechi. Halafu ikafungwa bao 1-0 na Fanja Club, leo imetoka suluhu ya bila kufungana na Seeb Club.
COASTAUNION

No comments:

Post a Comment