STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 6, 2014

'Simba hatuhusiki uvunjwaji wa viti Taifa'

UONGOZI wa Klabu ya Soka ya Simba umesema kuwa hauhusiki na vurugu za kuvunja viti zilizotokea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati Yanga inacheza mechi yake ya mabingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, Al Ahly ya Misri.
Simba ilisema jana kuwa imeamua kutoa taarifa hiyo kutokana na kuwapo kwa 'uvumi' kwamba klabu hiyo huenda ikapigwa faini kufuatia baadhi ya mashabiki wake kudaiwa kuvunja viti siku ya mchezo huo.
Baadhi ya picha zilizoonekana kwenye vyombo vya habari zilionyesha mashabiki waliovaa jezi nyekundu na wengine njano wakirushiana viti na kuacha kushangilia.
Afisa Habari wa klabu hiyo, Asha Muhaji, alisema kuwa mashabiki wa Simba hawawezi kuvunja viti kwa sababu mechi hiyo ilikuwa inawahusu wapinzani wao, Yanga na Al Ahly.
Muhaji alisema kuwa si kila shabiki aliyevaa jezi nyekundu ni wa Simba kwa sababu rangi hiyo inavaliwa na klabu mbalimbali za hapa nchini kama Coastal Union, Small Simba na Al Ahly iliyokuwa inashiriki mchezo huo.
"Sisi tunaamini waliofanya vurugu ni mashabiki wa Al Ahly ambao ndio walikuwa na wapinzani wa Yanga, inashangaza Simba tunatajwa kuhusika na vurugu hizo katika mechi tusiyokuwa na maslahi nayo," alisema Muhaji.
Aliongeza kwamba Simba inataka kuweka wazi kuwa vurugu zilizofanyika katika mchezo huo haziwezi kuhusishwa na klabu yao kwa namna yoyote.
Mara kadhaa mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, amekuwa akisisitiza mashabiki wa soka kuwa wazalendo pale timu mojawapo inapokuwa inapeperusha bendera ya nchi kushangilia na kuacha mazoea ya kuzomea.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema linaendelea kufanya uchunguiz juu ya tukio hilo kabla ya kutoa tamko, japo imelaani vurugu hizo na kuwaonya mashabiki kuwa wastaarabu kwa kuwa uwanja wa Taifa siyo wa klabu chache bali ni wa Watanzania wote.

No comments:

Post a Comment