MABINGWA wa zamani wa soka nchini, Coastal Union ya Tanga inatarajiwa kufanya Mkutano Mkuu wa wanachama Juni 22 kwenye ukumbi wa Hotel ya Mkonge, jijini Tanga, huku wakiwasainisha wachezaji kadhaa wapya na wa zamani kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa klabu hiyo, Oscar Assenga mkutano huo utakuwa na ajenda kuu mbili zitakazojadiliwa na mengineyo.
Assenga alisema ajenda ya kwanza itakuwa ni kupokea taarifa na kujadili taarifa za kazi kutoka kamati mbalimbali za utendaji ndani ya klabu hiyo kwa kipindi kilichopita.
Pia alisema kutakuwa na kuthibitisha bajeti kwa mwaka wa fedha unaofuata baada ya mwaka uliopita kumalizika ambapo mkutano huo hautaruhusu wanachama wanaodaiwa madeni kuhudhuria.
“Pia tutafanya marekebisho ya katiba kwani tutaongeza kifungu cha kamati ya maadili ambacho ni muhimu ikiwa ni agizo la TFF," alisema Assenga.
Afisa Habari huyo alitoa wito kwa wanachama wa klabu hiyo waliopo sehemu mbalimbali hapa nchini kuhakikisha wanatimiza haki yao ya msingi kwa kuhudhuria kwenye mkutano huo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya timu hiyo kongwe hapa nchini.
Mkutano huo unafanyika huku klabu hiyo ikiwa imeanza mchakato wa usajili wa wachezaji kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ikiwasainisha wachezaji kutoka Mgambio JKT, ASAhanti United na wale iliyoikuwa nao msimu uliopita, licha ya kukimbiwa na aliyekuwa mfadhili wao, Nassor BinSlum aliyeingia mkataba wa kuidhamini klabu ya Mbeya City kwa miaka mitatu.
No comments:
Post a Comment